Na MWANDISHI WETU, DODOMA
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amewashukuru na kuwapongeza madaktari wa Taasisi ya Bilal Muslim Tanzania ambayo imetoa huduma ya matibabu ya macho kwa zaidi ya wananchi 4,000 mkoani Dodoma.
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa pongezi hizo jana mjini hapa, wakati alipokuwa akizungumza na madaktari waliotoa huduma hiyo walipomtembelea katika makazi yake mjini Dodoma.
Waziri Mkuu Majaliwa alisema kwamba, huduma inayotolewa na taasisi hiyo ni muhimu, kwa kuwa imewezesha watu ambao walikata tamaa ya kuona, kuanza kuona.
Kutokana na hali hiyo, aliwaomba waendelee kwenda katika maeneo mengine nchini ili Watanzania wengi zaidi waweze kunufaika na huduma yao.
“Nawashukuru kwa mchango mkubwa mnaoutoa katika kuunga mkono jitihada za Serikali kwenye utoaji wa huduma za matibabu ya macho bure na kuwawezesha hata wale wasiokuwa na uwezo wa kupata huduma.
“Serikali ya awamu ya tano ina dhamira ya dhati kuwatumikia wananchi na kutoa huduma kwa wote, hivyo tuko tayari kushirikiana na taasisi yoyote inayokusudia kuwafikia wananchi.
“Katika utoaji wa huduma za kijamii, Serikali inathamini sana mchango wa taasisi binafsi na za dini ambazo ziko mstari wa mbele kushirikiana na jamii kwa ujumla,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwakaribisha madaktari hao kuja kuwekeza katika sekta mbalimbali mkoani Dodoma, kwa kuwa ndiko yaliko makao makuu ya Tanzania.
Naye Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Anthony Mavunde, alisema watoto 250 wamefanyiwa upasuaji wa macho na madaktari hao ambao walianza kutoa huduma hiyo Desemba 8, mwaka huu.
“Nawashukuru kwa moyo wenu wa kujitolea kuja kusaidia watu wenye mahitaji ya matibabu ya macho.
“Mkoa wa Dodoma una changamoto kubwa ya matatizo ya macho, nimefarijika sana kuona baadhi ya akinamama waliokuwa wamekata tamaa ya kuona, wameweza kuona tena,” alisema.