Na Abdallah Amiri-Nzega
WALIMU wakuu wa shule za msingi na sekondari wilayani Nzega mkoani Tabora wamelalamikia vitendo vya baadhi ya wazazi wilayani humo kuwatisha wanapohimiza wanafunzi kusoma kwa bidii na kukataa ndoa za utotoni.
Wakizungumza katika kikao kazi cha wadau wa elimu mwishoni mwa wiki, walisema baadhi ya wazazi hawataki watoto wao wasome shule hali inayosababisha uhasama mkubwa kati na wazazi.
Mwalimu Mkuu wa Shule Msingi Isilyaza, Sellema Juma alisema baada ya kutoka matokeo ya darasa la saba alifanya kikao na wanafunzi ndipo walipothibitisha kuwa baadhi ya wazazi waliwakataza watoto wao kujibu vizuri mitihani ya taifa waweze kufeli ili waolewe.
Alisema licha ya kufanya hivyo wazazi wamekuwa vikwazo kwa kukwamisha juhudi zinazofanywa na walimu za kuhakikisha elimu inapanda wilayani humo.
Juma alisema baadhi yao wamekuwa wakitoa vitisho kwa walimu ikiwamo kuuawa kwa imani za ushirikina.
“Ndugu zangu walimu nimetishiwa kuuawa na baadhi ya wazazi lakini pia wanafunzi wamethibitisha kukatazwa na wazazi kutofanya vizuri katika mitihani ya taifa,” alisema Mwalimu Juma.
Mwalimu Ramadhani Khalidi wa Shule ya Msingi Mambali alisema alishawahi kutishiwa kuuawa na baadhi ya wazazi kwa kuwaongeza muda wa ziada wa masomo wanafunzi wa shule yake .
Alisema Serikali inapaswa kutoa elimu hasa kwa wananchi wa vijijini waweze kutambua muhimu wa elimu kwa watoto wao.
Akijibu malalamiko hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega, Jacob Mtaritinya alisikitishwa kusikia malalamiko hayo kwa walimu wakuu.
Aliwataka kutokata tamaa na ofisi yake itachukua hatua za makusudi kukomesha vitendo hivyo vinavyofanywa na baadhi ya wazazi.
Ofisa Elimu wa Wilaya hiyo, Revocutus Mande aliwataka walimu wakuu kusimamia taaluma kwa wanafunzi kwa kutoa mitihani ya majaribio ya wiki huku changamoto zote walizoziorodheshwa zikiendelea kufanyiwa kazi.