27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

ZITTO APATA PIGO

ONE PK DATA Bericht

Na AGATHA CHARLES – DAR ES SALAAM

ALIYEKUWA Katibu wa Bunge na Serikali za Mitaa katika Sekretarieti ya Chama cha ACT-Wazalendo, Habibu Mchange, amejiondoa uanachama wa chama hicho na kujiweka kando na siasa.

Taarifa ya uamuzi huo wa Mchange ilisambazwa jana katika mitandao ya kijamii, ikionyesha kuandikwa naye huku ikiambatanishwa na namba yake ya simu.

Katika andiko hilo, Mchange aliyewahi kuwa mwanachama wa Chadema kabla hajahamia ACT Wazalendo, alisema aliamua kujitoa rasmi katika ushiriki wa aina yoyote ya siasa ili apate muda zaidi wa kusimamia shughuli zake za kijasiriamali.

Mchange alisema ameamua kujiengua na siasa ili kutoa fursa na huduma sawa kwa viongozi na wanachama wa vyama vyote vya siasa.

“Kwa moyo mkunjufu kabisa na kwa mapenzi mema na taifa langu, ninathibitisha kwamba nimejitoa rasmi katika ushiriki wa aina yote ya siasa ili nipate muda mwingi zaidi kufanya na kusimamia shughuli zangu za kijasiriamali zinazonitaka nitoe fursa na huduma sawa kwa viongozi na wanachama wa vyama vyote vya siasa,” alisema Mchange.

Alisema kutokana na uamuzi huo ambao aliomba uheshimiwe, lolote atakalolifanya lisihusishwe na chama bali iwe ni msimamo wake mwenyewe kama mtu huru asiye na chama.

“Ninafahamu kuwa mwanachama wa chama cha siasa ni haki yangu ya kikatiba, lakini nimeamua kuihifadhi kwa sasa mpaka hapo nitakapoona inafaa kufanya vinginevyo. Ninawatakia kila la heri waliokuwa wanachama wenzangu wa ACT Wazalendo katika kuyafikia malengo ya msingi ya uanzishwaji wa chama hicho,” alisema Mchange.

Mchange alisema kujiondoa kwake kusihesabiwe kama sehemu ya kukwamisha au kurudisha nyuma matarajio na au malengo ya chama hicho bali ichukuliwe kama chachu ya kufika mbali.

“Msivunjike moyo, msirumbane, pendaneni, heshimianeni na shikamaneni ili mfikie lengo. Nitabaki na kuendelea kuwa ndugu yenu, rafiki na swahiba. Zaidi Mtanzania mwenzenu. Tutaendelea kushirikiana katika mambo yote ya kijamii na kimaisha yasiyohusiana na mlengo wa kiitikadi wa kisiasa,” alisema Mchange.

Mchange alishika nafasi mbalimbali katika chama hicho ikiwamo Katibu wa Mipango na Mikakati, Mjumbe wa Kamati Kuu, Mjumbe wa Halmashauri Kuu na Mjumbe wa Mkutano Mkuu.

MTANZANIA Jumapili lilimtafuta Mchange kwa simu kuthibitisha andiko hilo, lakini hakuweza kupatikana.

Alipotafutwa Ofisa Habari wa ACT-Wazalendo, Abdallah Khamis, alikiri andiko hilo kuwa ni la Mchange.

Mchange anakuwa mwanasiasa wa tatu kuondoka ACT-Wazalendo mwaka huu baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Samson Mwigamba kuachia nafasi yake na kwenda masomoni nchini Kenya, Aprili mwaka huu.

Miezi michache baadaye, Novemba mwaka huu mwanasiasa Moses Machali naye alitangaza kujiondoa rasmi chama hicho na kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais Dk. John Magufuli.

Machali aliwahi kuwa Mbunge wa Kasulu Mjini kupitia Chama cha NCCR-Mageuzi kabla ya mwaka jana kushindwa kutetea jimbo lake kupitia ACT-Wazalendo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles