29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

TUANDAE VIJANA KUWA VIONGOZI SI WATAWALA

Hayati Mwalimu Nyerere
Hayati Mwalimu Nyerere

KABLA ya kuanza kuandika kile ambacho nimekikusudia kwa leo, nianze kwa kutoa pole kwa wananchi wa Cuba, kufuatia msiba mzito uliowapata wa kumpoteza rais wa zamani wa nchi hiyo, Komredi Fidel Castro.

Hayati Castro ni mmoja wa viongozi ambao walijitoa sadaka kwa ajili ya wananchi wake, pia kiongozi huyo aliamua kujitoa sadaka kwa ajili kupigania haki za wananchi wa mataifa mengine ambao walikuwa wakinyanyaswa na sera za nchi za magharibi, Afrika ikiwa ni mojawapo ya mhanga mkubwa.

Tangu akiwa kijana pamoja na mdogo wake Raul, Castro alionyesha kuwa atakuwa mmoja wa viongozi wa kutumainiwa na si taifa lake pekee, bali dunia nzima na hivyo ndivyo ilivyokuwa kwake hadi pale alipoamua mwenyewe kuachia hatamu ya uongozi wa Cuba.

Mengi yameandikwa kumhusu kiongozi huyo mashuhuri, Wacuba wamepoteza baba, babu, rafiki, mjomba, tumuenzi kiongozi huyu kwa vitendo kuhusu yale ambayo amekuwa akiyasimamia tangu akiwa msituni hadi kuwa kiongozi wa nchi. Pumzika kwa amani Komredi Castro.

Wiki iliyopita niliandika makala kuhusu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Paul Makonda. Katika makala hiyo niligusia namna Mkuu huyo wa Mkoa anavyowavuruga wasaidizi wake.

Nilipokea simu na ujumbe mfupi wa maneno (sms) kutoka kwa wanasiasa, viongozi wa dini, watumishi wa Serikali katika nafasi nyeti, wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa pamoja na wasomi mbalimbali.

Simu hizo pamoja na sms zilikuwa za kunipongeza kwa namna ambavyo nilijaribu kuzungumza kwa uwazi namna kiongozi huyo asivyowatendea haki wasaidizi wake pamoja na viongozi mbalimbali.

Nilichojifunza ni kuwa, tumeacha misingi imara iliyoasisiwa na viongozi wa taifa hili ya kuandaa vijana kuwa viongozi wa kesho, badala yake tumeshuhudia vijana wakipewa nafasi wanaishia kuwa watawala badala ya kuwa viongozi.

Kuna tofauti kubwa baina ya mtawala na kiongozi, mtawala anaweza kuwa mtu yeyote yule ambaye anaweza kupewa dhamana ya kusimamia eneo fulani na akafanikiwa kwa staili yoyote ile pasipo kufuata misingi ya utawala bora, haki, utawala wa sheria.

Tofauti na kiongozi, ambaye sifa yake kuu ni kufuata misingi ya sheria, utawala bora, haki, si mtu wa kujikweza, mnyenyekevu na hubebwa na sifa kuu ya kutokujikweza.

Tangu utawala wa awamu ya kwanza wa Mwalimu Julius Nyerere, kiongozi huyo alijitahidi kuandaa vijana kwa ajili ya kuwa viongozi bora wa hapo baadaye, aliliona hilo kuwa ni jambo la msingi na lilikuwa ni mojawapo ya vipaumbele vyake.

Mwalimu Nyerere kwa kutumia wasaidizi wake walikuwa na jukumu la kuhakikisha wanafuatilia mienendo ya vijana katika shule za msingi, sekondari, vyuo na katika vyombo vya ulinzi na usalama.

Lengo lilikuwa ni kupata vijana makini na wazalendo ambao watakuja kuisaidia Tanzania miaka ijayo wakiwa viongozi katika maeneo mbalimbali, kuna orodha ndefu ya vijana ambao waliibuliwa na utaratibu huo wa Mwalimu Nyerere.

Kazi hiyo ya Mwalimu iliwaibua kina Abdurahaman Kinana, Jakaya Mrisho Kikwete, Joseph Warioba, Samwel Sitta, Salim Ahmed Salim na wengineo.

Tangu wakiwa vijana hadi leo hii kwa wale ambao wako bado hai, viongozi hao wamefanikiwa kuishi kwa maadili yale yale, tofauti na vijana wa leo ambao wameshindwa kuonyesha utumishi uliotukuka na kujikita katika kutafuta umaarufu binafsi kupitia migongo ya wenzao.

Kundi hilo la vijana wa zamani niliowataja walikuwa hawahangaiki kutukana viongozi wenzao au kuwafedhehesha ili wao waonekane bora, viongozi hao walijikita katika kusimamia haki na kumwakilisha kwa vitendo aliyewapa dhamana ya kuongoza kwa niaba yake.

Nashukuru Watanzania wenzangu wameona tunakoelekea si kuzuri, na wameanza kutoa matamko katika vyombo vya habari na katika mitandao ya kijamii, wakikemea unyanyasaji na udhalilishaji unaofanywa na baadhi ya viongozi, lakini matamko pekee hayasaidii kujenga au kurekebisha jambo fulani.

Ili tuweze kufikia malengo, ni muhimu turejeshe utaratibu wa kuandaa vijana kuwa viongozi wa kesho kwa kuwajengea misingi imara ya uzalendo na uadilifu na tuache kushabikia mambo ya hovyo.

Nasema tuache kushabikia mambo ya hovyo kwa sababu vyama vya siasa vimechangia kuharibu maadili na uzalendo kwa baadhi ya vijana wetu, vijana wamejikuta wakipoteza maadili na uzalendo, wanachokitazama ni kuona watafanikiwa vipi kufikia malengo wanayoyataka.

Tujiulize kundi la vijana la kina Makonda, Sugu, Bulaya, Zitto Kabwe, Kafulila, Machali, Hamud Shaka na wengineo, vijana hawa wameharibiwa na wanasiasa kwa ajili ya malengo ya kisiasa.

Ni mara chache sana utawasikia vijana hao wakitetea maslahi ya nchi, siku zote wamekuwa wakitanguliza maslahi yao binafsi kwa malengo yao binafsi na wako tayari kufanya chochote ili mradi walichokilenga wamekipata, hata kama ni kwa gharama za vijana wenzao na watu wanaowazunguka.

Huwezi kupata viongozi bora miongoni mwa vijana kwa staili ya kulinda maslahi binafsi, tutapata vijana ambao tutawapa maelekezo ya kwenda sehemu fulani kutawala ili kile tunachokilenga kitimie.

Bado tuna vijana wengi ambao tunaweza kuwaandaa kwa ajili ya kuivusha Tanzania ijayo, kutokana na mabadiliko yanayoikumba dunia, jambo la kuandaa vijana wazalendo na waadilifu tunapaswa kulipatia kipaumbele zaidi.

Tanzania si kisiwa kwamba mabadiliko yanayotokea ulimwenguni hayawezi kuathiri nchi, mabadiliko yanayotokea katika nyanja mbalimbali yanaweza kuiathiri Tanzania endapo hatutakuwa na vijana wazalendo na waadilifu.

Ndiyo maana Mwalimu Nyerere kwa kuona umuhimu wa kuandaa vijana kwa ajili ya Tanzania ijayo, aligoma kujiingiza kichwa kichwa katika uchimbaji wa madini pamoja na uendelezaji wa rasilimali mbalimbali.

Aliona moto uliopo mbele pasipo kuandaa rasilimali watu, moto huo ndio ambao nauona tusiporejea kuandaa vijana katika misingi ya uzalendo na uadilifu, vijana hawa tusipowafunga gavana, iko siku wataichafua Tanzania na kusababisha amani kutoweka.

Naomba kuwasilisha.

 [email protected]

 0767 642602, 0784 642602

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles