NA AGATHA CHARLES, DAR ES SALAAM
RAIS Dk. John Magufuli ameteua mabalozi 21, kati yao wapya 15, wakiwamo wanasiasa wenye majina makubwa.
Mabalozi hao walioteuliwa ili kujaza nafasi zilizokuwa wazi katika balozi za Tanzania zilizoko nchi mbalimbali duniani, miongoni mwao ni wanasiasa maarufu, Dk. Emmanuel Nchimbi, Dk. Pindi Chana na Rajab Luhwavi ambao ni wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Luhwavi anayeshikilia wadhifa wa Naibu Katibu Mkuu Bara, CCM na Dk. Chana ambaye ni Kaimu Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Mambo ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa) pia ni wajumbe wa Sekretarieti ya chama hicho.
Taarifa ya uteuzi huo ilitolewa jana na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi na kusambazwa kwenye vyombo vya habari na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais-Ikulu, Gerson Msigwa.
Hata hivyo, taarifa hiyo haikuchanganua nchi ambazo mabalozi hao watapelekwa zaidi ya kutaja orodha ya nchi zilizo wazi na nyingine sita ambazo Tanzania imefungua balozi zake mpya.
Mbali na akina Nchimbi, wengine walioteuliwa ni Balozi Mbelwa Kairuki, ambaye ni mume wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angela Kairuki, Balozi Samuel Shelukindo, Balozi Silima Haji na Balozi Abdallah Kilima.
Wengine ni Balozi Joseph Sokoine ambaye ni mtoto wa Waziri Mkuu wa zamani, hayati Edward Sokoine, Balozi Baraka Luvanda na Balozi Dk. James Msekela aliyewahi kuwa mbunge wa Tabora na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na Dodoma.
Katika orodha hiyo, wamo pia Sylvester Ambokile, Luteni Jenerali mstaafu, Paul Mella, Grace Mgovano, Mohamed Bakari na Job Masima.
Kundi hilo linawajumuisha pia aliyepata kuwa Waziri wa Fedha katika Serikali ya awamu ya nne, Omar Yusuf Mzee, Matilda Masuka, Fatma Rajab, Sylvester Mabumba ambaye aliwahi kuwa mbunge wa Dole na mwenyekiti katika Bunge la 10, Profesa Elizabeth Kiondo na George Madafa (ambaye uteuzi wake ulishatangazwa).
Licha ya taarifa hiyo ya Ikulu kusema kuwa vituo vya kazi vya mabalozi hao 21 vitatangazwa baadaye, lakini iliviorodhesha vile vinavyohitaji wawakilishi hao kuwa ni Beijing-China, Paris-Ufaransa, Brussels-Makao Makuu ya Jumuiya ya Nchi za Ulaya, Muscat-Oman, Roma-Italia, New Delhi-India na Pretoria-Afrika Kusini.
Vituo vingine ni Nairobi-Kenya, Brasilia-Brazil, Maputo-Msumbiji, Kinshasa-Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Kampala-Uganda, Abuja-Nigeria, Moroni-Comoro na Geneva-Umoja wa Mataifa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Ikulu, mabalozi sita watakwenda katika balozi mpya zitakazofunguliwa hivi karibuni katika nchi za Algeria, Israel, Korea ya Kusini, Sudan, Qatar na Uturuki.
“Wale waliobaki katika vituo ambavyo si kati ya 15 vilivyotajwa, wataendelea na nafasi zao za uwakilishi katika vituo walivyopo,” ilieleza taarifa hiyo ikimnukuu Balozi Kijazi.
HESABU KALI
Uteuzi wa wanasiasa kama Dk. Nchimbi, Dk. Chana na Luhwavi ambaye ni mmoja wa waliofanya kazi kwa ukaribu na Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, akipata kuwa mmoja wa wasaidizi wake, umetoa taswira ya kufanyika kwa mabadiliko makubwa ndani ya CCM, hususani Kamati Kuu na Sekretarieti katika uchaguzi wa chama hicho utakaofanyika mwakani.
Si hilo tu, uteuzi wa Dk. Nchimbi, ambaye amekuwa mjumbe wa miaka mingi wa CC, wakati fulani akipata kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM, Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Naibu Waziri na baadae Waziri katika wizara mbalimbali, nao umetoa taswira kwamba sasa Rais Magufuli anajenga CCM moja.
Kitendo cha Rais Magufuli kutomteua Dk. Nchimbi katika Serikali yake kilizua maswali mengi.
Julai, mwaka jana Dk. Nchimbi akiwa na wajumbe wenzake wa Kamati Kuu ya CCM, Sophia Simba na Adam Kimbisa, walijitokeza mbele ya vyombo vya habari na kudai kujitenga na uamuzi wa chombo hicho kwa kuwa kilikiuka Katiba ya CCM wakati wa mchakato wa kupata jina la mgombea urais.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amemhamisha Balozi Modest Mero kutoka kituo chake cha sasa cha Geneva, kwenda Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) yaliyopo New York-Marekani, ambako atakuwa mwakilishi wa kudumu wa Tanzania.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa Balozi Mero anachukua nafasi ya Balozi Tuvako Manongi ambaye atastaafu Desemba 6.
Pia Rais Magufuli amemteua Grace Martin kuwa Balozi na Mkurugenzi wa Itifaki (Chief of Protocal) – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Kikanda na Kimataifa. Uteuzi huo wa Grace aliyekuwa akikaimu nafasi hiyo ulianza jana.
Wengine walioteuliwa ni Balozi Peter Kallaghe ambaye sasa anakuwa Ofisa Mwandamizi Mwelekezi – Mambo ya Nje katika Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC).
Kabla ya uteuzi huo, Balozi Kallaghe alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza hadi mwanzoni mwa mwaka huu.