GENEVA, USWISI
KAMISHNA wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa (UN), Zeid Ra’ad Al Hussein, ameitaka Serikali ya Tanzania kuchunguza na kuwashtaki watu waliohusika na uhalifu wa mauaji dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino).
Al Hussein amehoji vitendo hivyo kujitokeza wakati nchi ikiwa inaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.
Tamko hilo alilitoa jana ambapo alilaani vikali mauaji ya mtoto albino Yohana Bahati mwenye umri wa mwaka mmoja.
“Nalaani vikali mauaji haya ya kutisha na ukataji viungo vya Yohana Bahati, mtoto albino mwenye umri wa mwaka mmoja kaskazini mwa Tanzania,” alisema.
Jumapili iliyopita, Yohana alitekwa kutoka kwa mama yake na watu watano wasiojulikana waliokuwa na silaha za jadi, hasa mapanga na mama yake alijeruhiwa vibaya wakati akijaribu kumwokoa.
Mwili wa mtoto huyo uliokotwa Februari 17 ukiwa hauna mikono wala miguu.
Al Hussein, alisema mashambulizi dhidi ya albino, mara nyingi huchochewa na matumizi ya viungo vyao vya mwili kwa ajili ya ushirikina, ambapo hadi sasa yamegharimu maisha ya watu 75 nchini Tanzania tangu mwaka 2000.
Alisema mashambulizi hayo yanaonekana kuzidi kuongezeka katika miezi miwili ya karibuni, ambayo imeshuhudia wastani wa matukio matatu kila mwezi.
“Mashambulizi na ukandamizaji dhidi ya watu albino yasitishwe mara moja na ninatoa wito kwa mamlaka za Tanzania kuchunguza na kuwashtaki wahusika wa uhalifu huu mbaya na kuimarisha hatua za ulinzi kwa watu wenye ulemavu wa ngozi, hasa kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu,” alisema Al Hussein.
ALBINO WAOMBA HIFADHI
Akizungumza na MTANZANIA jana jijini Mwanza, Mwenyekiti wa Chama cha Albino mkoani humo, Alfred Kapole, alisema kutokana na vitendo vya ukatili na utekwaji wa watoto wawili albino kwa kipindi cha miezi miwili, wamezidi kuingiwa hofu na kupoteza imani ya kuendelea kuishi nchini.
Alisema hivi sasa wapo kwenye mchakato wa kukutana albino wote nchi nzima ili kutafuta hifadhi kwenye nchi yoyote kwani inaonekana Serikali imeshindwa kuwalinda na kutoa adhabu kali dhidi ya wahusika.
“Hii imekuwa ni ‘changa la macho’, kila ikitokea albino kafanyiwa ukatili Serikali inasema imeimarisha ulinzi na kujinadi kwamba hakuna tukio jingine litakalotokea tena, lakini baada ya muda linaibuka tukio jingine.
“Bado tuna majonzi ya mtoto Pendo Emmanuel aliyetekwa Desemba 27, mwaka jana na hajapatikana, hatujui yuko wapi na kama yu hai au ameuawa. Juzi tena mtoto wa mwaka mmoja naye ameporwa na kuuawa, jamami hivi tuna raha gani ya kuendelea kuishi hapa nchini?” alisema na kuhoji.
Kutokana na hali hiyo, Kapole alitupa lawama kwa wanasiasa kwa kushindwa kutekeleza makubaliano ya mwaka 2008 ya kukemea mauaji ya albino na kuhamasisha jamii iachane na imani potofu kila wanapofanya mikutano na wapigakura wao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Under The Same Sun (UTSS), Vicky Ntetema, alilaani vikali vitendo hivyo na kuiomba jamii kubadili mtazamo wa imani za kishirikina kwa kuwa hakuna mtu anayepata utajiri kupitia viungo vya albino.
SERIKALI YATANGAZA VITA
Kutokana na matukio hayo ya mauaji dhidi ya watu wenye albino, Serikali mkoani Mwanza imetangaza msako dhidi ya watu ambao wanahusishwa nayo.
Hayo yalisemwa jana na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Baraka Konisaga, ambapo alisema Serikali imejipanga kupambana na watu hao kwa nguvu ya aina yoyote na kuwafikisha katika vyombo vya dola.
“Hili tukio la mtoto Yohana Bahati kutekwa na kuuawa limetokea mkoani Geita, kabla ya tukio hilo itakumbukwa liliwahi kutokea wilayani Kwimba mkoani Mwanza baada ya mtoto Pendo Emmanuel (4) kutekwa.
“Natangaza rasmi kuanzia leo mapambano yanaanza kuwatafuta wahusika, tutatumia kila mbinu kwa kuwatumia watuhumiwa wawili wanaoshikiliwa na polisi ili kubaini mtandao huo,” alisema Konisaga.