25.6 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Wakili aliyemtesa ‘housegirl’ anyimwa dhamana

Dar es Salaam
Eneo la katikati ya Jiji la Dar es Salaam

MANENO SELANYIKA NA FABIAN NDAKI

WAKILI wa kujitegemea, Yasinta Rwechungura (44) anayekabiliwa na kesi ya kumtesa, kumpiga na kumnyanyasa mfanyakazi wake wa ndani, Merina Mathayo, amenyimwa dhamana.

Rwechungura amenyimwa dhamana kwa kuwa hali ya binti huyo bado ni mbaya na anaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Akiwasilisha hoja za kuomba kupatiwa dhamana jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, Wakili anayemtetea Rwechunguza, Godion Isaya, alidai mbele ya Hakimu Boniphace Lihamwike kuwa mteja wake kisheria ana haki ya kupatiwa dhamana.

“Mheshimiwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema kuwa dhamana ni haki ya kila mtu hivyo ninaomba mteja wangu apewe dhamana kwa kuwa nimejiridhisha kuwa atakuwa salama kwani hakuna mtu yeyote wa kumdhuru akiwa nje ya Mahakama.

“Lakini pia mshitakiwa kwa kuwa ni mara yake ya pili kuja mahakamani, ana wadhamini wa kuaminika pia wenye anuani zinazoeleweka mahali na sehemu sio tu wanapoishi lakini pia wanapofanya kazi,” alidai Wakili Isaya.

Kwa upande wa Jamhuri uliokuwa ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Mohamed Salum uliendelea kusimamia hoja zake na kuitaka Mahakama isimpatie dhamana wakili huyo kwa madai kuwa Mkuu wa Upelelezi Kinondoni (R.C.O) alitoa kiapo cha maandishi kuwa mshitakiwa asipewe dhamana kutokana na kesi inayomkabili kwani vitendo vya kuwatesa wafanyakazi wa ndani vimekithiri.

“Kwa mujibu wa sheria za makosa ya jinai kifungu cha 148 (5) (d) sehemu hii inasema kuwa ni haki kisheria mshtakiwa kupewa dhamana lakini kuna mazingira ambayo lazima dhamana izuiliwe hivyo kutokana na hali ilivyo tunaiomba Mahakama hii tukufu izidi kuzuia dhamana yake,” alidai Salum.

Upande wa Mahakama baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili ilionekana kuridhishwa na hoja za upande wa Jamhuri na kusisitiza kuwa kiapo kilichotolewa na R.C.O kuwa mshitakiwa asipatiwe dhamana ni cha msingi.

“Jalada lililoko mikononi mwangu hapa halina nyaraka zote kwa kuwa Hakimu aliyekuwa amekabidhiwa kesi hii amehamishiwa kituo cha kazi kingine hivyo ninaomba kesi hii ipangwe tarehe fupi kwa ajili ya mapitio ya hoja zilizowasilishwa hapa leo ili kujiridhisha na maamuzi zaidi,” alidai Hakimu Lihamwike.

Hata hivyo kesi hiyo ambayo kwa mara ya kwanza ilisomwa kwa Hakimu Suleiman Mnzava, ambaye kwa mujibu wa Mahakama hiyo kwa sasa amehamishwa sehemu nyingine, ilichukua takribani saa mbili kupangiwa Hakimu mwingine huku wanaharakati, wananchi pamoja na waandishi wa habari wakiwa nje ya Mahakama hiyo hadi mshitakiwa alipotolewa mahabusu kuingia mahakamani.

Kesi iliahirishwa hadi Julai 4 mwaka huu ili kuipa Mahakama muda wa kupitia vizuri hoja za pande zote mbili na pia kupangiwa kwa Hakimu mwingine.

Wakili huyo kwa mara ya kwanza alifikishwa katika Mahakama hiyo Juni 17 mwaka huu akikabiliwa na shtaka la kumjeruhi Merina Mathayo (15) aliyekuwa akifanya kazi za ndani nyumbani kwake Boko Njiapanda nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles