Na HERIETH FAUSTINE – DAR ES SALAAM
JESHI la Polisi Kanda ya Kinondoni linawashikilia wafanyabiashara watatu kwa uuzaji wa shisha ambao ulipigwa marufuku na Serikali kwa vile una madhara kwa watumiaji.
Hatua hiyo imekuja baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kumtuhumu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Polisi Kinondoni, Suzzana Kaganda.
Makonda alidai huenda viongozi hao walipokea rushwa ya Sh milioni 50 kutoka kwa kikundi cha wafanyabiashara 10, hali iliyosababisha kushindwa kuwakamata wauzaji wa kilevi hicho.
Makonda alitoa tuhuma hizo akisema rushwa hiyo ndiyo inawafanya Sirro na Kaganda walegelege kuwakamata wafanyabiashara hao waliomfuata ofisini kwake, licha ya kuwaagiza kufanya hivyo.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kamanda Sirro alisema wafanyabishara hao walikamatwa wakiwa na vielelezo ambavyo vinatarajiwa kupelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi.
“Watu watatu ambao ni wafanyabiashara wa shisha wamekamatwa wakiwa na vielelezo na taarifa zaidi anazo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Polisi Kinondoni,”alisema Sirro.
MTANZANIA, lilimtafuta Kamanda Kaganda ambaye alikiri kukamtwa wafanyabiashara hao wa shisha usiku wa kuamkia jana katika maeneo ya Mikocheni.
Alisema kupitia operesheni wanayoendelea kuifanya ya kuwasaka wafanyabiashara wa kilevi cha shisha, waliwezaa kuwakamata watatu wakiwa na mashine za shisha
Alisema kutokana na upelelezi unaoendelea kufanywa kuhusiana na biashara hiyo, kwa sasa hawataweza kuyataja majina yao kwa kuhofia kupoteza ushahidi.
Kamada alisema wafanyabiashara hao kwa sasa wanashikiliwa na polisi kwa mahojiano katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay.