Na Kulwa Mzee -Dar es Salaam
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imesema haimwogopi Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), bali wanaomwogopa ni Jamhuri ambao walipewa hati ya kumkamata lakini hawakufanya hivyo.
Hayo yalisemwa jana na Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Thomas Simba, wakati kesi ya uchochezi inayomkabili Lissu na wenzake watatu ilipokuwa ikitajwa na Lissu kuonekana mahakamani.
Wakili wa Serikali, Patrick Mwita, alidai jana kesi ilikuwa inatajwa, upande wa utetezi ama mshtakiwa Lissu aeleze kwanini dhamana yake isifutwe kwa kushindwa kufika mahakamani mara mbili.
Alisema mdhamini si mbadala wa mshtakiwa, hivyo aliomba mahakama iheshimiwe na itekeleze jukumu lake la kufuta dhamana.
Kutokana na kauli hiyo ya wakili wa Serikali, hakimu Simba alisema: “Hati ya kumkamata ilitolewa na wewe ukiwapo, hamkumkamata mshtakiwa, leo unasema anaidharau mahakama, nanyi Jamhuri mmeonyesha dharau kwa kutomkamata wakati mlikuwa na wajibu wa kumkamata… sijui mnamwogopa.
“Nafasi yako Lissu ni sawa na washtakiwa wengine, unasafiri hutoi taarifa, usituingize katika migogoro, wewe ni kiongozi, hatukuogopi labda Jamhuri ndio wamekuogopa, nilitoa amri ukamatwe hawakukukamata, hatupambani na wewe tunataka ufuate utaratibu.
“Hatukuonei wala kukuogopa, waliokuleta mahakamani wameogopa kukukamata, wasitake tufikie hatua ya kuishikilia hati yako ya kusafiria, ili kila ukitaka kusafiri ufike kuiomba mahakamani,” alisema Hakimu Simba na Wakili Mwita aliomba radhi mahakama kwa kushindwa kumkamata Lissu.
Mwita aliomba kuahirisha kesi hiyo na Wakili wa utetezi, Peter Kibatala, aliomba kuondoa nia ya kukata rufaa kupinga washtakiwa hao kusomewa shtaka la kwanza na la tano.
Mahakama ilikubali kuahirisha kesi hiyo hadi Desemba 20, mwaka huu kwa kutajwa.
Mbali na Lissu, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mhariri wa Gazeti la Mawio ambalo lilifungiwa na Serikali kwa muda usiojulikana, Simon Mkina, mwandishi Jabir Idrisa na mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama kuchapisha chapisho la uchochezi, kuchapisha taarifa ya uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.
Wanadaiwa kutenda makosa hayo, kati ya Januari 12 na 14, mwaka huu, jijini Dar es Salaam. Kwamba kwa pamoja waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho ‘Machafuko yaja Zanzibar’.