KUWA kwenye uhusiano pekee hakutoshi ila kuwa katika uhusiano imara, wenye dira ni jambo bora zaidi. Baadhi ya marafiki huanzisha uhusiano lakini baada ya muda huachana na kubaki na maumivu moyoni.
Mwingine hujikuta akianzisha uhusiano kila wakati na kuacha, kuachwa au kuachana na mpenzi wake kutokana na sababu za hapa na pale.
Lakini ukitazama kwa undani utagundua kuwa kuvunjika kwa uhusiano kwa wengi husababishwa na kutokuwa na maarifa ya namna gani unaweza kuwa bora kwenye uhusiano wako.
Kwa mfano wanaume wamekuwa si watu wa kujali sana mambo ya uhusiano wao. Wanachukulia mambo kwa wepesi tu, tofauti na wanawake ambao asilimia kubwa hutafuta mbinu za kuwa na uhusiano bora kila wakati.
Baadhi ya wanaume wamejikuta wakiwa kwenye uhusiano usiyo na afya au kufikia hatua ya kukimbiwa na wanawake au kuwa sababu ya kuachana bila ya wao kujua.
Katika mada hii iliyoanza wiki iliyopita, ninachambua sababu ambazo zinaweza kumfanya mwanamke asifikirie kuachana na mwanamume kabisa.
Kwa maneno mengine niseme kuwa, naeleza mambo muhimu ambayo mwanamke anayahitaji kwa mwanamume wake na asifikirie kamwe kuachana naye. Tayari tumeshaona baadhi ya mambo hayo katika matoleo yaliyopita.
Sasa tumalizie sehemu hii ya mwisho ya mada hii.
KUPEWA KIPAUMBELE
Kuna wakati wanawake huwa na mambo yao binafsi. Kazini au kifamilia. Inawezekana akatatizika katika eneo fulani ambalo kwa namna moja ama nyingine atahitaji usaidizi wako. Ikitokea mkeo akawa katika hali hiyo, msikilize.
Mathalani ana tatizo la kifamilia, amekuambia mmoja wa wazazi wake anaumwa, msaidie. Si lazima kifedha, lakini kuonesha kujali kwako tu, kutampa matumani kwamba anaishi na mtu sahihi. Acha kupuuza mambo yake; hata yale madogo, kama ya ‘mtoto wa dada amerudishwa ada shuleni’.
Msikilize, mshauri panapofaa kufanya hivyo na ukiweza msaidie hata kifedha. Katika upande wa pili ni hivyo hivyo. Labda una tatizo binafsi, kazini kwako au kifamilia, mshirikishe.
Unaweza kushangaa jambo ambalo uliamini unaweza kulimaliza peke yako, kwa kumshirikisha likawa jepesi zaidi na mambo yakaendelea vyema. Kipaumbele kwa namna yoyote ile, kunaongeza mapenzi zaidi kwa mwanamke.
TENDO LA NDOA
Hiki ni kipengele nyeti, kinachohitaji lugha nzuri ya kirafiki kukifafanua. Hakuna siri, tendo la ndoa ni moja ya kiwakilishi cha ndoa. Maana hata maandiko yanasema: “Mwanamke ataacha wazazi wake na kwenda kwa mumewe, nao watakuwa mwili mmoja.”
Kimsingi tendo la ndoa lina nafasi yake. Ni muhimu likaheshimiwa na kutengewa muda maalum wa kufurahia. Si papara. Kwa bahati mbaya wanaume huwa si wafuatiliaji sana wa kujua namna ya kuwafurahisha zaidi wenzao. Wenyewe wanajiwazia wenyewe. Wanafikiria namna ya kuwakomoa wenzao.
Si sahihi. Tendo la ndoa halina maana ya kukomoana. Jenga mazoea ya kufanya maandalizi kamili kabla ya tendo. Sikiliza hisia za mwenzako. Ukiweza kumjulia mke wako katika eneo hili, ni wazi kwamba utazidisha upendo wake kwako, lakini pia atakuwa katika kuta za uaminifu. Akatafute nini nje wakati wewe ndiye mganga wake unayeweza kumtibu barabara?
Nikuache na neno moja; uamuzi wa kuijenga ndoa yako upo mikononi mwako. Ukitaka iwe shaghalabaghala, pia ni wewe tu!
Je, unahitaji kupata masomo haya zaidi kupitia group letu la WhatsApp? Karibu inbox kwa namba zangu hapo chini, sema tu unataka kuungwa kwa group letu, nitakuunganisha.
Jiandae kupata kitabu changu kipya cha SIRI ZA NDOA YENYE FURAHA. Kama unakihitaji weka oda yako kupitia 0712 170745 (What’sApp na sms tu).