25.8 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Tanzania ilivyoibuka kidedea mashindano ya Hisabati

Wanafunzi Taasisi ya SIP Abacus & Brain Gym ya jijini Dar es Salam ambao waliibuka washindi
Wanafunzi Taasisi ya SIP Abacus & Brain Gym ya jijini Dar es Salam ambao waliibuka washindi

Na FARAJA MASINDE,

ELIMU ni ufunguo wa maisha! Hili liko wazi na linapaswa kutambuliwa na wazazi wote, pia waone umuhimu wa kuwekeza kwenye elimu ya watoto tangu wakiwa wadogo kwa maana ya kuwajengea msingi bora wa elimu.

Hata hivyo, utafiti unaonyesha kuwa wazazi wengi wamekuwa hawapendi kuwapa msingi bora watoto wao kwenye nyanja ya masomo hasa yale ambayo wao binafasi hawakufanya vizuri au walifeli.

Masomo ya sayansi hasa somo la Hisabati ni miongoni mwa masomo ambayo yamekuwa yakikimbiwa na wanafunzi wengi kutokana na kile wanachodai kuwa ni magumu na hawawezi kuyamudu.

Wanafunzi wengi wanadai kukosa hamasa, kutokuwapo kwa walimu wa kutosha na sababu zingine lukuki zinazotolewa na wanafunzi wa kileo.

Changamoto hizo ndizo zilizoisukuma Taasisi ya SIP Abacus & Brain Gym kuanzisha programu maalumu kwa watoto wadogo wenye umri wa kuanzia miaka sita hadi 10 ili kuwajengea msingi bora wa somo la Hisabati.

Katika kudhihirisha mafanikio ya mpango huo, wanafunzi wanaosoma masomo hayo ambayo yako nje ya ratiba ya shule wameibuka kidedea kwenye mashindano ya somo la Hisabati yaliyofanyika nchini Sri Lank yakihusisha nchi 18.

Mmiliki na mkufunzi wa kituo hicho kilichopo Upanga jijini Dar es Salaam, Sapha Bhattbhatt, anasema mashindano hayo yalihusisha somo la Hisabati ambapo mwanafunzi alitakiwa kujibu maswali 50 ndani ya dakika tatu.

Anasema Tanzania iliibuka kidedea kupitia wanafunzi wa kituo hicho ambao walizawadiwa medali za dhahabu pamoja na kikombe.

Sapha anasema mashindano hayo yameipa heshima kubwa Tanzania kutokana na kuwa na vijana wenye vipaji vya juu kwenye somo la hisabati ambao wana uwezo mkubwa wa kujibu maswali ya papo hapo bila kuhusisha kikokotozi.

“Mashindano haya yalikuwa kama ilivyo Olympic, ambapo watoto kutoka mataifa 18 walishiriki kujibu maswali 50 ya hesabu ndani ya dakika tatu, Tanzania ilifanya vizuri ambapo Mahek Desai (7) alishinda kombe huku Treasure Beda (7) na wengine watano wakishinda medali za dhahabu.

“Mpango huu licha ya kwamba naufanya kwa jitihada zangu binafsi lakini umekuwa na mafanikio makubwa kwani watoto wengi ambao wamekuwa wakipitia kwenye mafunzo haya wamekuwa wakifaulu kwa kiwango cha juu katika mitihani yao ya hesabu.

“Licha ya kuwa mwamko wa wazazi bado ni mdogo lakini haijanivunja moyo kwani matokeo chanya yamekuwa yakionekana kila kukicha, hivyo tunataka kufuta dhana hii ya kwamba hesabu ni somo gumu,” anasema Sapha.

Anasema kwasasa kituo hicho kina walimu 10 ambao wanafundisha somo la hesabu tu kwa wanafunzi hao mara tu baada ya kutoka shule, huku akisisitiza kuwa kuwafundisha hesabu watoto wadogo inakuwa rahisi kuliko wakiwa watu wazima.

“Haya ni sawa tu na mazoezi ya ubongo ambayo humjengea mtoto uwezo wa kitu kukaa kichwani bila kusahau kuhusu hesabu za aina zote. Mbali na kuwajengea uwezo huo wa hesabu pia mafunzo haya yanawapa kasi ya kuandika na kujibu maswali kwa haraka zaidi ikilinganishwa na wanafunzi ambao hawasomi mafunzo haya.

“Kila darasa ni lazima liwe na wanafunzi 15 ili kuhakikisha kuwa wanakuwa na uelewa mzuri darasani,” anasema.

Kulingana na mkufunzi huyo, zaidi ya wanafunzi 500,000 kutoka duniani kote wamenufaika na mpango huo kwani umeongeza uelewa wao kujiamini katika kufanya hesabu na uwezo mkubwa wa kuhifadhi vitu.

Anasema mpango huo wa Abacus ni mfumo wa kujifunza hesabu ulioanzishwa na walimu wa China zaidi ya miaka 2000 iliyopita ambao unawasaidia wanafunzi kufanya hesabu bila kutumia kikokotozi huku ukisisimua ubongo kufanya kazi kwa haraka.

“Malengo yangu ni kuona mafunzo haya ambayo yana ngazi ya kwanza mpaka ya tatu yanawafikia wanafunzi wengi zaidi nchini licha ya kuwa wazazi wengi wamekuwa wazito kuwaleta watoto wao,” anasema.

Wazazi

Josephine Manege ambaye ni mzazi wa mwanafunzi Treasure, anasema mpango huo ni mzuri na kwamba jambo hilo linapaswa kufanywa na wazazi wote kwani linawasaidia kuwajengea uwezo wa kujibu maswali ya hesabu.

“Tumekuwa tukijenga dhana ya kuamini kuwa hesabu ni ngumu lakini huu ndio wakati mzuri wa kuwajengea uwezo watoto wetu ili kuwajengea uwezo wao hasa kwenye somo hili.

“Pia mkakati huu unapaswa kuungwa mkono na serikali kwani una manufaa makubwa kwa taifa, unawafanya wanafunzi waimarishwe zaidi kwenye somo la hesabu na hivyo kutayarisha wataalamu wa baadaye,” anasema Josephine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles