Na JOSEPH HIZA,
IWAPO unadhani wakati unapoelekea kazini asubuhi hii umekumbana na adha mbalimbali ikiwamo foleni, kugombea kupanda au kushonana ndani ya daladala, na kadhalika, angalia safari hizi za kila siku za watoto wakielekea shule.
Kuanzia kudandia waya kuvuka Mto Rio Negro nchini Colombia hadi kuning’inia katika daraja lililobomoka nchini Indonesia, wanafunzi wanahatarisha maisha yao kila siku wakati wakiisaka elimu.
Kama wewe ni mwanafunzi, ambaye unapata shida kama hizo ikiwamo kuzuiwa, kusukumwa na makondaka kisa nauli yako ndogo, huku ukitamani kuwa kama wale watoto kutoka familia zinazojiweza ambazo wanaenda shule kwa usafiri wao, fikiria watoto wengine kama hawa.
Kwamba katika baadhi ya maeneo duniani kote, suala la kwenda shule ni kitu cha kuumiza mno zaidi ya vile unavyoumiza kichwa kufikiria namna usafiri utakavyokuwa wakati ukienda au kurudi kutoka kazini.
Hali kama hizo ni moja ya sababu kuu zinazofanya wanafunzi wengi duniani kuacha shule.
Lakini pia kuna wengine wenye ujasiri na dhamira ya kuendelea kupata elimu, wakiangalia manufaa yao ya baadaye licha ya mazingira hatarishi ya njia za kuelekea shule.
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi na Elimu (UNESCO), mafanikio ya kuwaunganisha watoto na shule kipindi cha miaka kadhaa iliyopita yalishuka.
Moja ya njia au usafiri wa kuelekea shule ni pamoja na ile inayofanya kushonana kwa abiria ndani ya daladala kuwa cha mtoto, kwa vile nchini India kuna kijiji, ambacho wanafunzi 35 hujazana kama kuku katika kigari kidogo cha kukokotwa na farasi wakielekea shule.
Nyingine ni kudandia tube za matairi kuwavusha mtoni hadi kuendesha punda kwa saa tano katika njia myembamba na hatari milimani.
Nyingine ni namna watoto wa Shule ya Msingi katika Kijiji cha Gulu, Jimbo la Sichuan, China, ambao huvuka njia nyembamba mno pembezoni mwa majabali na miamba wanapoenda na kurudi shule.
Awali hakukuwa na mtu nje ya kijiji hicho aliyekuwa akijua shule hiyo inayohudumia kijiji hicho kwa miaka 60 hadi gazeti moja  liliporipoti habari zake miaka sita iliyopita.
Wafadhili wakamiminika ili kuwasaidia watoto wasome katika shule zilizoko mjini chini ya mlima, lakini baadhi walibaki kijijini kwa sababu familia zao hazikuwa na uwezo wa kulipia malipo ya kila mwezi.
Nyingine ni njia ambamo wanafunzi huvuka Mto Ciherang karibu na kijiji chao cha Lebak Regency nchini Indonesia.
Kutokana na kuanguka kwa upande mmoja wa msingi wa daraja, kulisababisha lining’inie upande na hivyo wanafunzi kutembea kwa staili ya kudandia upande.
Nchini Colombia, ili kuwawahisha shule watoto na wanakijiji pia hutumia waya unaowapitisha kuvuka Mto Rio Negro nchini Colombia.
Familia hizo huishi maili 40 kusini mashariki mwa mji mkuu wa Colombia wa Bogota, hutumia waya huo kuwakutanisha na dunia iliyowatenga.
Iko futi 1,300 juu ya Mto Rio Negro na wasafiri huvuka mto kwa kasi ya maili 40 kwa saa kufika ukingo wa pili, ulio nusu maili.
Watoto wanaoishi katika Kijiji cha Zhang Jiawan, kilipo juu milimni katika Jimbo la Hunan, China, wanalazimika kupanda ngazi zisizo salama zilizoegemea jabali lenye urefu wa mita 60 kila siku wanapoenda na kurudi shule.
Ngazi hizo zinazotengenezwa na wanakijiji zimekuwa zikibadilishwa kila baada ya miaka mitatu hadi minne. Kama si ngazi hizo njia mbadala ya kufika shule ni safari ya saa nne.