KOKU DAVID NA ESTHER MNYIKA, DAR ES SALAAM
RAIS Dk. John Magufuli jana aliongoza waombolezaji wengine kuaga mwili wa aliyewahi kuwa Waziri wa Elimu na Ufundi, Joseph Mungai katika Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam.
Mwanasiasa huyo mkongwe alifariki dunia Novemba 8, mwaka huu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Viongozi wengine waliotoa heshima za mwisho kwa mwanasiasa huyo ni Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, mawaziri wakuu wastaafu, Frederick Sumaye na Jaji Joseph Warioba.
Mwili wa Mungai unatarajia kusafirishwa leo kuelekea kijijini kwao Mafinga mkoani Iringa kwa mazishi yatakayofanyika Jumamosi.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, atamwakilisha Rais Magufuli katika mazishi hayo.
Wakati wa kuaga mwili wa Mungai, Rais Magufuli alishindwa kujizuia kutokwa machozi.
Kingunge amkumbuka
Mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale Mwiru, alisema kuwa alimfahamu marehemu kwa miaka mingi tangu enzi za chama cha TANU na baadaye CCM.
“Katika nyadhifa zote alizoshika alikuwa kiongozi mwenye akili na mchapakazi, alijituma na ndiyo sababu iliyochangia kuchaguliwa kuwa waziri wa kwanza kijana katika Baraza la Mawaziri la Serikali ya awamu ya kwanza.
“Mungai alikuwa na kichwa kizuri, pia alikuwa mchapakazi na mzalendo, alipenda wananchi wake katika majimbo yake na ndiyo maana katika Mkoa wa Iringa alijenga shule za sekondari zipatazo 12, zilizokuwa chini ya familia yake, ambazo baadaye aliamua kuzikabidhi kwa Serikali,” alisema Kingunge.