29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Mke wa Magufuli alazwa Muhimbili

Rais Dk. John Magufuli, akimjulia hali mke wake, Mama Janeth Magufuli, ambaye amelazwa Wodi ya Sewa Haji katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam jana.
Rais Dk. John Magufuli, akimjulia hali mke wake, Mama Janeth Magufuli, ambaye amelazwa Wodi ya Sewa Haji katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam jana.

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

MAMA Janeth Magufuli, mke wa Rais Dk. John Magufuli, amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) akipatiwa matibabu.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa Wateja hospitalini hapo, Aminiel Eligaesha, alithibitisha kwamba   mgonjwa huyo alipokewa juzi.

“Ni kweli tumempokea Mama Janeth jana (juzi) mchana na amelazwa wodini, lakini hatuna mamlaka ya kutaja yupo katika wodi gani na hata ugonjwa unaomsumbua ni siri yake na daktari wake… au labda umpigie msemaji wa Ikulu, wanaweza kukueleza,” alisema.

Kwa mujibu wa walioshuhudia mgonjwa huyo akifikishwa Muhimbili, kwa nyakati tofauti walisema ulinzi ulikuwa mkali, alibebwa na uongozi wa wauguzi wa hospitali hiyo akapelekwa Kitengo cha Huduma za Dharura.

“Mke wa Rais Magufuli alifikishwa hapa hospitalini, madaktari wengi walishirikiana kutoa huduma na baadaye alilazwa katika Wodi ya Sewahaji Private kwa matibabu.

“Madaktari na wauguzi walikuwa wakihaha mpaka usiku kuhakikisha anapatiwa matibabu ya haraka,” alisema mtu huyo na kupongeza juhudi za madaktari na wauguzi.

Hata hivyo ilipofika saa 7.00 mchana, muda ambao kwa kawaida ni wa kuona wagonjwa waliolazwa hospitalini hapo, MTANZANIA lilishuhudia msafara wa magari uliokuwa umembeba Rais Magufuli ukiwasili.

Msafara huo ulikwenda moja kwa moja hadi katika Jengo la Sewahaji ambako Rais  na wasaidizi wake walishuka na kuingia ndani ya wodi hiyo.

Askari walionekana kuimarisha ulinzi kuzunguka jengo hilo na hata ndugu waliokuwa wakiingia kupeleka chakula kwa wagonjwa wao nao walizuiliwa.

Baadaye ndugu hao walielezwa na walinzi kuwa ndani ya jengo hilo aliingia Rais Magufuli ambaye alikwenda kumjulia hali mkewe.

Kauli hiyo iliwafanya ndugu waliokuwa wamebeba vyakula kushangaa, huku wakieleza kuwa hawajawahi kusikia mke wa kiongozi mkubwa kama huyo kulazwa hospitalini hapo.

“Kwa kweli Rais Magufuli ni wa pekee, viongozi wengine wanakimbilia nje ya nchi, lakini yeye mke wake amekuja kulazwa hapa, ni heri tuwe na subira tusubiri kidogo amuone kisha na sisi tuingie,” alisikika mmoja wa ndugu hao akizungumza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles