29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Kilichomwangusha Clinton hiki hapa

Hillary Clinton
Hillary Clinton

Na JUSTIN DAMIANI, ALIYEPO MAREKANI

MFANYABIASHARA mwenye utata, bilionea Donald Trump, jana alichaguliwa kuwa Rais wa 45 wa Marekani, huku akiwaacha baadhi ya Wamarekani na duniani kote wakiwa hawaamini kilichotokea.

Trump anakuwa Rais wa kwanza wa taifa hilo kubwa duniani ambaye hajawahi kuwa mtumishi wa umma wala kufanya kazi jeshini.

Ushindi wa Trump umekuwa ni mshutuko hapa Marekani na Wamarekani wengi bado wanajiuliza nani amempigia kura mgombea huyo kupitia chama cha Republican ambaye amekuwa akionekana kama siyo mtu ‘makini’kugombea nafasi hiyo kubwa.

Rais anayemaliza muda wake, Barrack Obama, aliwahi kumrushia ‘kijembe’ kwenye kampeni kwamba Wamarekani hawawezi kumchagua Rais ambaye hata akaunti yake ya Twitter tu ilimshinda kuisimamia.

Trump ameshinda kiti cha Urais baada ya kushinda majimbo muhimu ya Florida, North Carolina na Ohio. Wakati wa uchaguzi, nilipata nafasi ya kutembelea takriban vituo 15 vya kupigia kura hapa North Carolina. Katika mahoijiano niliyofanya na wapiga kura zaidi ya 38, walionekana kutomkubali hata kidogo. Kati ya watu wote niliofanya nao mahojiano ni mmoja tu ambaye alikuwa mgombea kupitia chama hicho ambaye pia alisema Trump hakuwa chaguo lake lakini atamchagua kwa sababu anatoka kwenye chama chake.

Ingawa North Carolina ni miongoni mwa majimbo yenye ushindani mkubwa, mara nyingi  jimbo hili limekuwa likiangukia kwa Democrat  jambo ambalo limekuwa tofauti kwa uchaguzi wa mwaka huu.

Kitendo cha Democrat kushindwa uchaguzi kwa mgombea ambaye alioneaka ni ‘kibonde’ kitakifanya chama hicho  kilichokuwa kikipewa nafasi kubwa ya kurudi Ikulu kwa awamu ya tatu  kuomboleza kwa muda mrefu

Ingawa historia ya Marekani inaonyesha   chama kilichopo madarakani mara chache sana kurudi madarakani baada ya miaka minane, Democrat walikuwa na nafasi kubwa ya kushinda kiti hicho kutokana na aina ya mgombea mpinzania wao alivyokuwa.

Clintoni aliweza kumshinda Trump katika mdahalo wa pili uliofanyika Las Vegas kwa alama11 lakini baada ya kashfa ya pili ya barua pepe ushindi huo ulishuka mpaka kufikia alama nne.

Pamoja na jitihada za timu yake kulibana Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) kutoa majibu ya kashfa hiyo na baadaye kufanya hivyo na kumsafisha siku mbili kabla ya uchaguzi huo, bado Trump alisisitiza kuwa FBI wamelazimishwa kutoa majibu haraka  kumsafisha Hillary.

Katika kampeni zake, Clinton hakuweza kuyapa uzito wa kutosha mataizo makubwa yanayowakabili Wamarekani wengi kama mishahara midogo na kukosekana kwa usawa.

Trump alifanikiwa kuwashawishi Wamarekani kuwa matatizo hayo yanasababishwa na mikataba mibovu ya biashara  na uchumi mbovu na vyote alisema yeye anayo dawa yake.

Mafanikio makubwa ya biashara aliyonayo Rais huyo mpya, yanaweza kuwa ni moja ya sababu ya wapiga kura kumwamini kuwa kama atatumia maarifa yaliyomfanya kufanikiwa kwenye biashara zake kwa kuhamasisha uwekezaji na biashara ndani na nje ya nchi pengine nchi inaweza kufika mbali.

Wapiga kura wa Wamerani wanaweza kuwa wamemchukulia mama huyo kama siyo mtu mwaminifu sana kutokana na kashfa ya asasi yao ya familia ambayo siyo ya biashara ya Clinton Foundation kujiingiza katika masuala ya biashara na kujitengenezea mamilioni ya dola kwa maslahi binafsi.

Clinton pia inawezekana akawa ameshindwa uchaguzi kwa kuwa vijana wengi hawakumchagua kwa sababu hakuwa na jambo maalum  kwa kundi hili ambalo linaathiriwa na ukosefu wa ajira.

Hiyo haina maana kuwa vijana walikuwa wanampenda Trump.  Kura za maoni ziliwahi kuonyesha kuwa vijana hawakuwa wanampenda Trump. Takriban theluthi  mbili ya    vijana walisema Trump hakuwa anafaa kuwa rais kwa vile ni mbaguzi na asiyethamini wanawake. Lakini badala ya kumpigia kura mgombea ambaye angemshinda, vijana wengi walisema wangewapigia wagombea wadogo ambao kwa hesabu wanampunguzia kura Clinton na kumwongezea Trump.

Ingawa Clinton aliweza kuchangisha fedha nyingi kwa ajili kampeni, hakuwa na ujumbe ambao ulibaki masikioni na mioyoni mwa wapiga kura wake watarajiwa.

Trump ambaye alikuwa ni fundi wa kucheza na vyombo vya habari alipopata nafasi, alikuwa akisema jambo ambalo watu hawakulitarajia na alikuwa akijiongezea wapiga kura kwa staili hiyo huku akiacha mijadala ambayo ilidumu kwa muda.

Ushindi wa Trump umekuwa si habari nzuri   kwa Wamarekani wenye msimamo wa wastani na kumekuwa na mjadala kama mgombea huyo atandelea kuwa na misimamo yake aliyokuwa nayo katika kampeni zake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles