Justin Damian, North Carolina
RAIS Barack Obama wa Marekani, amemtabiria wakati magumu mgombea wa chama chake cha Democratic, Hillary Clinton, endapo atachaguliwa kuwa rais wa kwanza mwanamke wa taifa hilo kubwa duniani.
Akizungumza katika mahojiano na kituo kimoja cha runinga jana, Rais Obama alisema Clinton atapitia wakati mgumu kama aliyopitia yeye akiwa rais wa kwanza mwenye asili ya Afrika.
Alisema Clinton anatakiwa ajiandae na hujuma kutoka kwa watu mbalimbali, ikiwamo mshindani wake bilionea Donald Trump.
“Watasema mengi tu kama vile amechoka, si mvumulivu, ana hasira sana na mengine mengi,” alisema Rais Obama.
“Wakati wanaume wakiwa na nia ya kufanya kitu kwa nguvu, inachukuliwa kama jambo la kawaida na watu wanasema ndivyo mwanaume anatakiwa awe. Lakini akiwa ni mwanamke watauliza kwa nini anafanya hivyo. Hili litamwandama kwa kipindi chote cha urais wake na inachangiwa na mtizamo kuwa amekuwa akificha jambo fulani,” alisema.
Akiwa katika hisia za sikukuu ya watakatifu wote (Halloween) ambayo huadhimishwa kila Oktoba 31 ya kila mwaka, Rais Obama alitania kwa kusema alikuwa amevaa kama itakavyotokea wakati vijana wakipiga kura na alisema kama hawatatokea kupiga kura Donald Trump anaweza kuwa rais.
Rais Obama alitokea kwenye kipindi cha runinga kufanya mahojiano ili kuwashawishi watu na hasa vijana kujitokeza kupiga kura.
“Vijana wanaonekana kuwa na mwamko mkubwa wa kupiga kura na tunapaswa kuwapongeza kwa hili, binti yangu mkubwa Malia amepiga kura kwa mara ya kwanza. Sifa kubwa aliyopata ni kuweza kupiga kura kumchagua kiongozi anayeona anamfaa,” alisema.
Alisema Clinton ana mpango maalumu kuhusiana na kupunguza gharama za kusoma vyuoni ambayo mpinzani wake hana. Vijana wana nafasi muhimu sana kwenye uchaguzi huu kuliko marika mengine. Ningependa kuona kila kijana badala ya kutumia muda wake kuangalia video kupitia simu yake ya mkononi, anakwenda kupiga kura.
Katika jitihada za kuwashawishi wapiga kura vijana kujitokeza kwa wingi, Rais Obama aliwafikia wapiga kura wa rika hilo kupitia mtandao wa kijamii wa snapchat Jumanne kupitia programu ya Good Luck America