Na Patricia Kimelemeta – Dar es Salaam
SHIRIKA la Nyumba na Taifa (NHC), limesaini mkataba wa mkopo wa Sh bilioni 65 kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB) kwa ajili ya kuendeleza mradi wa nyumba za kisasa, unaojulikana kama Seven Eleven uliopo Kawe, Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa NHC, Nehemiah Mchechu, alisema mradi huo unagharimu Sh bilioni 150, lakini kitendo cha kupewa mkopo huo kitasaidia kuuanzisha.
Alisema mkopo huo ni wa miaka saba na utatumika kwa ajili ya kujenga nyumba 422 kwa kushirikiana na wawekezaji wa sekta binafsi kutoka ndani na nje ya nchi.
“EADB imetoa mkopo wa Dola za Marekani milioni 30 ambazo ni sawa na Sh bilioni 65 kwa ajili ya kuendeleza mradi wa ujenzi huu,” alisema Mchechu.
Alisema NHC inategemea mkopo na uuzaji wa nyumba ili iweze kupata faida, hivyo basi kukamilika kwa nyumba hizo kutasaidia kupata wawekezaji.
Mchechu alisema mradi utakapokamilika utakuwa na huduma mbalimbali za kijamii, ikiwamo maduka na kumbi za burudani zitakazopatikana ndani ya saa 20 kwa siku.
Alisema kutokana na hali hiyo, mradi huo utakua kitovu cha biashara kutokana na huduma zitakazotolewa katika eneo hilo, jambo ambalo linaweza kubadilisha taswira ya Jiji la Dar es Salaam na kwendana na majiji ya mataifa mbalimbali kama vile Johannesburg lililopo nchini Afrika Kusini.
“Mradi wa Kawe ni mkubwa kuliko miradi mingine ya Dar es Salaam, una hekta 270 ambazo ni sawa na mita za mraba (square meters) milioni moja, na kwamba upo karibu na Bahari ya Hindi, tunaamini utakuwa mradi wa mfano kuliko miradi mingine,” alisema.