Na Mwandishi Wetu, Katavi
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, ameshuhudia uharibifu mkubwa wa mazingira katika Mto Katuma unaohatarisha maisha ya wanyama waliopo katika Hifadhi ya Taifa ya Katavi.
January alishuhudia uharibifu huo jana akiwa katika ziara yake mahususi ya kutambua na kufahamu changamoto za mazingira ikiwa ni siku ya 10 katika mwendelezo wa ziara ya siku 16 katika mikoa 10 na alipokea taarifa ya Mazingira ya Hifadhi ya Taifa ya Katavi kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Meja Jenerali mstaafu, Raphael Muhuga, iliyoainisha kuwa hali ya viboko, mamba na wanyama wengine wanaotegemea maji kwa maisha yao kuwa ni mbaya hasa kipindi hiki cha kiangazi kwa sababu maji ya mto huo yamepungua.
Baada ya kushuhudia uharibifu unaotishia kukausha mto huo, January, alisema hali hiyo ni tishio si tu kwa uhai wa Hifadhi ya Katavi ambayo ina twiga weupe wanaopatikana hifadhini hapo peke yake bali ni tishio kubwa kwa mazingira na maisha ya wote wanaotegemea na kutumia maji na rasilimali nyingine katika mto huo huku viboko na mamba wakipata shida zaidi kutokana na kupungua kwa maji.
Alipokagua eneo la chanzo cha mto huo, January, aligundua uchepushaji mkubwa wa maji unaofanywa na watumiaji wa mto huo waliopo juu (upstream) na kusababisha kupeleka kiasi kidogo cha maji kufika kwa watumiaji walioko chini (downstream) na alijionea uharibifu mkubwa wa mazingira unaotokana na shughuli za kibinadamu.
Kutokana na hali hiyo, aliagiza kufanyika kwa tathmini ya athari kwa mazingira kwa mto huo na kuuagiza uongozi wa Mkoa wa Katavi kuainisha baadhi ya maeneo yatakayotangazwa kama maeneo nyeti ili kunusuru mto huo na mazingira ya Katavi kwa ujumla lakini pia ametaka kuendelea kuondoa wavamizi wote waliovamia vyanzo vya maji na misitu, kuweka udhibiti wa uchepushaji wa maji ikiwamo kuvunja kabisa mabanio ya kienyeji yaliyowekwa na kusimamisha miradi ya umwagiliaji ya kienyeji inayochepusha maji.
“Tumeongea na uongozi wa mkoa kuchukua hatua madhubuti kabisa kutibu tatizo hili lililosababisha mto huu kukauka, ninafahamu kuna hatua zimeshaanza, tunataka hatua hizo ziendelee na tutaziunga mkono lakini pia tutachukua hatua nyingine mpya,” alisema January.