Na SARAH MOSES, DODOMA,
WAJUMBE wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), wameitaka Halmashauri ya Jiji la Arusha kuwasilisha vielelezo vya matumizi ya fedha za mradi wa mkakati wa uendelezaji majiji (AGB) kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kabla ya Novemba 30, mwaka huu ili yakahakikiwe.
Agizo hilo lilitolewa jana mjini hapa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Abdallah Chikota kwa niaba ya wajumbe wa kamati hiyo.
Kwa mujibu wa Chikota, kutokuwapo kwa vielelezo vya miradi hiyo ni dalili ya kutotekelezwa kwa miradi husika.
Pia, kamati hiyo iliitaka Halmashauri ya Jiji la Arusha kutotumia fedha za Mfuko wa Vijana na Wanawake kwa kuwa haijaridhiswa na taarifa za mkurugenzi wa jiji hilo aliyesema ametumia Sh bilioni 1.6 kwa matumizi mengine.
Kwa upande wake, Mbunge wa Ulyankulu, John Kadutu (CCM), alisema miradi hiyo inatakiwa kukaguliwa kwa kuwa inaonekana haijatekelezwa kama ilivyotarajiwa.
“Baadhi ya miradi ambayo haijatekelezwa mpaka leo ni ujenzi wa choo, ujenzi wa mifereji na mradi wa usafi wa mazingira wa Jiji la Arusha.
“Ndiyo maana nasema kuna haja CAG aikague ili tuone maendeleo yake na jinsi fedha zilivyotumika kwa sababu tumeshaanza kuwa na mashaka,” alisema Kadutu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashari ya Jiji la Arusha, Athumani Kihamia, alisema jiji hilo halijafikia malengo kwa kuwa hakuna tathmini ya kodi za majengo, hakuna vyanzo vipya vya mapato na kuna ubadhirifu wa fedha za umma unaofanywa na baadhi ya watumishi wasiokuwa waadilifu.