Na EDITHA KARLO,
SERIKALI mkoani Kagera imesema  tathimini iliyofanyika  ya athari za tetemeko la ardhi mkoani hapo imebaini ujenzi wa makazi ya watu kurejea kwenye hali yake kunahitaji   Sh bilioni 880 huku ujenzi wa miundombinu  ya serikali ukihitaji Sh bilioni tisa.
Mkuu wa Mkoa Kagera, Meja Jenerali (mstaafu), Salum Kijuu, aliyasema wakati akipokea msaada wa fedha na vitu mbalimbali yakiwamo mablanketi na vyandarua kutoka kwa taasisi ya Adra Tanzania ya Kanisa la Adventisti Tanzania lenye makao makuu yake   Arusha.
Kijuu alisema hadi sasa fedha zilizoingizwa katika akaunti ya maafa ya Kagera ni   Sh bilioni nne  ambazo hazitoshelezi katika ujenzi wa makazi ya watu.
Alisema  serikali imependekeza vifaa vingine vipelekwe katika taasisi za umma vikiwamo vituo vya afya na  shule  wananchi waendelee kupata huduma kama ilivyokuwa awali.