Na MASYENENE DAMIA
WAZIRI wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba amewaasa wakulima wa mazao mchanganyiko kuchangamkia kilimo cha dengu kwa kuwa soko lake ni kubwa nje nchi.
Dk. Tizeba alitoa kauli hiyo juzi alipozungumza na MTANZANIA akisema soko la dengu ni kubwa India na tayari Serikali ya Tanzania imeingia makubaliano ya awali ya kununua zao hilo.
Alisema katika makubalino hayo, India imeahidi kununua tani kuanzia milioni mbili hadi sita kutegemea uwezo kiasi kilichozalishwa na wakulima hapa nchini.
“Kama kuna wananchi wanataka kuchangamkia kilimo hiki basi wafanye hivyo maana soko lipo, mataifa ya Asia yanahitaji sana dengu zetu kwahiyo tuna soko la uhakika kwa wakulima wetu.
“India kuna soko kubwa la dengu na wanahitaji sana , waziri mkuu wao alifunga safari kuja kutuomba tuwauzie dengu.
“Kwa sasa tunazalisha tani milioni 1.6 za dengu na mazao mengine mchanganyiko yakiwamo choroko na mbaazi,” alisema.
Dk. Tizeba alisema mkakati wa serikali ni kutengeneza soko litakalowahamasisha wakulima kulima na kuzalisha zaidi kuongeza uwezo wa uzalishaji wa nchi.
Alisema Serikali imeweka mazingira kwa wakulima wa zao hilo ambao hawana mitaji kwenda benki ya NMB kukopeshwa mitaji ya kuanzisha shughuli za kilimo cha dengu.
Waziri alisema bado kuna uwezekano wa wananchi kuzalisha tani milioni tatu mpaka nne na kuwasihi kuwasihi wananchi kuzalishe zaidi kwa sababu soko la dengu lina uhakika.
Alisema makadirio ya mauzo ya dengu kwa mwaka jana nchini iliweza kuuza choroko, dengu na kunde zenye thamani Sh bilioni nne.