NA TUNU NASSOR, DAR ES SALAAM
MBUNGE wa Kibamba, John Mnyika (Chadema), ametoa madawati 537 yenye thamani ya Sh milioni 64.4 katika kata sita za jimbo hilo ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa ya uboreshaji wa huduma za elimu.
Akikabidhi madawati hayo kwa madiwani wa kata za jimbo hilo kwa niaba ya mbunge, Katibu Msaidizi wa Mbunge, Liberatha Samson alisema katika kuyagawa kila kata imepata madawati 89.
Alisema ugawaji wa madawati hayo umezingatia ukubwa wa tatizo katika kata na shule husika ambapo awamu hii shule za msingi ndizo zimefaidika.
“Kata ya Saranga shule ya Msingi Saranga imepata madawati 34 na Shule ya King’ongo 55 na Kata ya Goba Shule ya Kulangwa imepata madawati 60 na Tegeta A imepata 29. Kata ya Mbezi Shule ya Mbezi imepata madawati 89,” alisema Liberatha.
Alisema Kata ya Msigani Shule ya Msingi Temboni imepata madawati 31, ambapo Shule ya Msigani madawati 29 na Maramba Mawili madawati 29.
“Kata ya Kwembe Shule ya Msingi Kingazi imechukua madawati 40 huku Shule ya Kwembe madawati 49, Kata ya Kibamba Shule ya Hondogo imepata madawati 44 na Kibwegere imepata madawati 45,” alisema Liberatha.
Liberatha aliongeza kuwa kupitia mfuko wa jimbo hilo wamefanikiwa kupata Sh milioni 39 ambazo zimegawanywa katika kata zote kuchochea shughuli mbalimbali za maendeleo.