27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Maisha ya madereva 10 waliotekwa DRC hatarini

Moja ya malori yaliyokuwa yakitokea Tanzania yaliyochomwa moto na waasi katika eneo la Nomoyo, Jimbo la Kivu Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambapo baadhi ya madereva walitekwa.
Moja ya malori yaliyokuwa yakitokea Tanzania yaliyochomwa moto na waasi katika eneo la Nomoyo, Jimbo la Kivu Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambapo
baadhi ya madereva walitekwa.

Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM

SERIKALI imeingilia kati na kuanza mazungumzo ya kuwaokoa madereva 12 wa malori kutoka Tanzania waliotekwa nchini Kongo (DRC) na kundi la waasi wa Mai Mai.

Waasi hao mbali na kuwateka madereva hao wametoa saa 24 kuanzia juzi saa 10 jioni walipwe fedha kiasi cha Dola za Marekani 4,000 kwa kila dereva ili waweze kuwaachia.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mindi Kasiga, alisema waasi hao wametishia kuwaua mateka hao endapo hawatalipwa kiasi hicho cha fedha hadi kufikia jana saa 10 jioni.

Mindi alisema katika tukio hilo, madereva wawili wa Kitanzania walifanikiwa kutoroka na ndiyo waliosaidia kutoa taarifa kuhusu tukio hilo.

“Serikali imepokea taarifa za kutekwa kwa malori 12 katika eneo la Namoyo Jimbo la Kivu Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, jana (juzi) Septemba 14,  2016. Kati ya malori hayo manane yanamilikiwa na mfanyabiashara wa Kitanzania, Azim Dewji na mengine yanamilikiwa na wafanyabiashara kutoka Kenya.

“Kwa taarifa zilizopatikana watekaji ni kikundi cha waasi cha Mai Mai ambao baada ya kuyateka magari hayo, waliwashusha madereva na kuwapeleka porini na kisha kuteketeza kwa moto malori manne ambayo yote ni ya Dewji.

“Waasi hao wametoa saa 24 kuanzia jana saa 10 jioni walipwe fedha kiasi cha Dola za Kimarekani 4,000 kwa kila dereva ili waweze kuwaachia,” alisema Mindi.

Alisema Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeshachukua hatua za awali za kuwasiliana na Serikali ya DRC ili kuhakikisha kuwa madereva hao wanaachiwa haraka iwezekanavyo wakiwa salama kabisa.

Alisema tukio la aina hiyo ni la pili kutokea ambapo katika mwaka jana masheikh kutoka Tanzania walitekwa nchini DRC lakini kwa ushirikiano wa Serikali hizo mbili juhudi ziliweza kuzaa matunda na masheikh hao kuachiwa huru bila madhara yoyote.

“Serikali ingependa kuushauri umma wa Watanzania hususan wafanyabiashara kuomba taarifa ya hali ya usalama kwa maeneo yenye matatizo ya kiusalama kama Mashariki ya Kongo hususan Kivu ya Kusini kabla ya kusafiri kwenda maeneo hayo,” alisema Mindi.

Kauli ya Azim

Akizungumza na MTANZANIA jana Mkurugenzi wa Kampuni ya Simba Logistics, Azim Dewji alithibitisha kutekwa kwa madereva wake.

Alisema tayari ubalozi wa Tanzania nchini Kongo na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki  wanashughulikia suala hilo.

Alisema tukio hilo limetokea sehemu inaitwa Kasebebena na Matete, wastani wa kilomita 30 kutoka mji wa Namoya nchini humo.

Aliyataja majina ya madereva waliotekwa na waasi hao wa Kundi la Mai Mai kuwa ni Hamdani Zarafi, Athuman Fadhili,  Juma Zaulaya, Adam James, Issa Idd Omary, Bakari Shomari, Hussein Mohamed na Mwamu Mbwana Twaha.

Kauli ya ACT-Wazalendo

Kutokana na hali hiyo Chama cha ACT -Wazalendo, kilisema kimepokea kwa mstuko taarifa ya kutekwa kwa Magari 12 ya kusafirisha mizigo yaliyokuwa safarini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Taarifa ilitolewa na Katibu wa Mambo ya Nje wa chama hicho, John Mbozu, ilieleza kuwa  moja ya malengo makuu  ni kuhakikisha Watanzania wanakuwa salama popote waendapo.

Taarifa ya Tatoa

Taarifa iliyotolewa na Chama cha Wamiliki wa Magari ya Mizigo Tanzania (Tatoa), ilieleza kwamba waasi wa Mai Mai  wa Kongo, wamewateka nyara madereva hao wa Tanzania na kuchoma baadhi ya magari ya mizigo.

Katika tukio hilo inaelezwa kuwa magari manne ya Tanzania yamechomwa moto na madereva wote walichukuliwa na waasi  ambapo tukio hilo limetokea sehemu inayoitwa Kasebebena na Matete, wastani wa kilomita 30 kutoka Mji wa Namoya.

“Tatoa  inawashauri wanachama waliopakia mzigo kuelekea huko kuwasiliana na madereva wao ili wasitishe safari, kusubiri taarifa ya hali ya usalama kutolewa,” ilieleza taarifa hiyo ya Tatoa.

Historia ya kundi la Mai Mai

Mai Mai Kata ni kundi la waasi nchini DRC ambalo linadai kupigania uhuru wa Jimbo la Katanga linaloongozwa na Gedeon Kyungu Mutanga, ambaye aliunda kundi hilo kutoroka gerezani mwaka 2011.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles