Veronica Romwald na Hadia Khamis, Dar es Salaam
VIRUTUBISHO vya madini ya ‘folic acid’ ambayo humkinga mtoto aliyeko tumboni asipatwe na tatizo la kichwa kikubwa vimeanza kuwekwa katika unga wa ngano.
Hatua hiyo imekuja baada ya Serikali kupitisha sheria inayowataka wazalishaji wa bidhaa hiyo kuongeza madini hayo, ili kukabili ongezeko la idadi ya watoto wanaozaliwa na tatizo hilo.
Hayo yalielezwa jana na Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI), Dk. Othumani Kiloloma, alipozungumza na waandishi wa habari juu ya awamu ya tatu ya upasuaji unaodhaminiwa na GSM Foundation ambao utafanyika katika mikoa mitano ya Tanzania Bara.
“Madini ya folic acid hupatikana zaidi kwenye matunda na mboga mboga kutokana na ukubwa wa tatizo serikali imeona vema kupitisha sheria hiyo na baadhi ya wazalishaji wa unga wa ngano wameanza kuongeza madini hayo,” alisema.
Alisema inakadiriwa kila mwaka watoto 4,000 huzaliwa na tatizo la kichwa kikubwa, lakini wanaofikishwa hospitalini ni watoto 500 pekee.
“Kwa hiyo watoto 3,500 hawafikishwi hospitalini, huko tunakopita tunajifunza mengi, wapo watoto ambao walikuwa wamepelekwa kwa waganga wa kienyeji wazazi wao wakihangaika kuwatibu na wengine walishindwa kufikishwa hospitali kutokana na sababu nyinginezo,” alisema.
Dk. Kiloloma alitaja mikoa mitano ambayo timu ya madaktari 10 wa MOI watafanya upasuaji huo ni pamoja na Pwani, Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Mara.
“Upasuaji utafanyika kwa siku tatu na tunatarajia kuwafanyia watoto 60 wapya katika kila mkoa na kuwafanyia matibabu wale ambao tulishawahi kuwafanyia maana na wenyewe huwa tunawapokea kila tunapokwenda na hii inawapunguzia mzigo wananchi kuwaleta Dar es Salaam kwa matibabu.
“Hivyo Pwani utaanza leo hadi 14, mwaka huu Hospitali ya Tumbi, Tanga katika Hospitali ya Bombo Septemba 16 hadi 18, Kilimanjaro Hospitali ya KCMC 20 hadi 22, Arusha Hospitali ya Mount Meru 24 hadi 26 na Mara Hospitali ya Musoma 28 hadi 30 Septemba, mwaka huu,” alisema.
Naye Ofisa Habari wa Kampuni ya GSM, Halfani Kiwambwa alitoa wito kwa jamii kuwafikisha watoto wenye matatizo katika hospitali hizo.