23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Shein awapa somo wakulima wa karafuu

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein.

Na Mwandishi Wetu-PEMBA

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amewahimiza tena wakulima wa karafuu kuendelea kuuza karafuu zao kwa Shirika la Taifa la Biashara Zanzibar (ZSTC), kwa kuwa kufanya hivyo kuna manufaa makubwa kwao binafsi na taifa kwa jumla.

Wito huo ameutoa jana alipokuwa akizungumza na watumishi wa ZSTC pamoja na baadhi ya wakulima wa zao hilo katika kituo kikuu cha karafuu Wilaya ya Mkoani.

Dk. Shein ambaye alifika kituoni hapo kuangalia maendeleo ya ununuzi wa karafuu pamoja na usafirishaji wake, alisema hatua madhubuti zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Saba zimerejesha tena hadhi ya zao la karafuu, hivyo wakulima hawana budi kuuza karafuu zao ZSTC ili kuendelea kulipa hadhi zao hilo.

“Tuliwatazama wakulima kwanza kwa kuwapatia bei nzuri na tukahakikisha kuwa biashara ya karafuu haibinafsishwi na ndio maana tukapitisha sheria kuwa Serikali ndiye mnunuzi pekee wa zao hilo,” alisema Dk. Shein.

Alisema uamuzi wa Serikali wa kuwapatia wakulima asilimia 80 ya bei ya karafuu katika soko la nje ulikuwa uamuzi unaothibitisha dhamira ya Serikali ya kuliendeleza na kulienzi zao hilo ambalo ni utambulisho wa Zanzibar.

“Tumechukua hatua muhimu za kulifanyia mabadiliko Shirika la ZSTC hadi kufikia na kuwa shirika lenye kutengeneza faida na kujiendesha lenyewe,” alisema.

Rais huyo aliwapongeza wakulima wote wanaoshirikiana na Serikali katika kuliendeleza zao la karafuu ikiwamo kuuza karafuu zao ZSTC pamoja na kuwafichua wananchi wanaoshiriki uhalifu wa kufanya magendo ya zao hilo.

“kutokana na ushirikiano wa wananchi, vitendo vya magendo ya karafuu mwaka jana vilishuka hadi kufikia chini ya asilimia tano,” alisema Dk. Shein.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wajumbe wa kikosi kazi pamoja na viongzoi wengine kuongeza kasi ya ufuatiliaji wa masuala ya karafuu ikiwamo kuangalia usalama wake wakati wote.

Awali Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko, Balozi Amina Salum Ali,  alimweleza Rais Shein kuwa msimu wa uchumaji na ununuzi wa karafuu unaendelea vyema hadi sasa na kubainisha kuwa walengwa wote wamewezeshwa kutekeleza majukumu yao.

Kwa upande wake, Ofisa Mdhamini wa ZSTC Pemba, Abdallah Ali Ussi, alisema hadi kufikia Septemba 9, mwaka huu shirika hilo limenunua jumla ya tani 1371.6 kisiwani Pemba ambazo ni sawa na asilimia 51 ya makisio ya manunuzi ya tani 2,650.

Alisema kati ya tani hizo 1157.6 zenye thamani ya Sh bilioni 16.2, tayari zimeshasafirishwa Unguja na tani 183 zenye thamani ya Sh bilioni 2.6, ziko katika kituo hicho cha Mkoani zikisubiri kusafirishwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles