24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, December 19, 2024

Contact us: [email protected]

Walazimika kupanda ndege kufuata kipimo cha ‘typhoid’ Dar

typhoid

NA GUSTAPHU HAULE, PWANI

WAGONJWA wa homa ya matumbo (typhoid), wilayani Mafia, wanalazimika kusafiri kwa ndege hadi Dar es Salaam kufuata tiba ya ugonjwa huo, kutokana na ukosefu wa kipimo hicho katika Hospitali ya Wilaya.

Hali hiyo inadaiwa kusababisha vifo vya wagonjwa wengi kutokana kushindwa kumudu gharama ya Sh 250,000 ambayo ni ya usafiri pekee.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Erick Mapunda, alitoa changamoto hiyo katika Kikao cha Ushauri cha Mkoa wa Pwani (RCC) kilichofanyika juzi mjini Kibaha, mkoani hapa.

Mapunda alisema mgonjwa anapokwenda hospitalini hapo hakuna huduma anayopata zaidi ya kuandikiwa ili aende kutibiwa jijini Dar es Salaam, jambo ambalo ni hatari kwa afya za wakazi wa halmashauri hiyo.

“Hospitali hii ni changamoto tuliyonayo hospitalini kwetu kwa wagonjwa wa typhoid, mgonjwa analazimika kuandikiwa ili aende bara kutibiwa.

“Lakini changamoto inayokuja watu hawana uwezo wa kusafiri kwa kuwa gharama za nauli pekee ya kwenda na kurudi ni zaidi ya 250,000,” alisema Mapunda.

Aidha, Mapunda aliiomba Serikali kupitia kikao hicho kuangalia suala hilo kwa umakini ili wananchi waliopo wilayani humo waweze kupata huduma ya tiba dhidi ya ugonjwa huo kiasi ambacho kitaweza kuokoa maisha yao.

Alisema mbali na hilo lakini pia bado hospitali hiyo inakabiliwa na changamoto ya kuwepo kwa miundombinu mibovu na ukosefu wa wahudumu wa afya huku akiomba mkoa kuongeza bajeti za kuboresha hospitali hiyo.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani (RAS),  Zuberi Samataba alisema atajenga hoja ili kuona jinsi ambavyo wataweza kupeleka watumishi  wa afya wilayani humo, lakini pia Serikali inaendelea kutoa fursa kwa Watanzania kusomea sekta ya afya ili waweze kusaidia katika maeneo wanayotoka.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo, akichangia hoja hiyo alisema Mafia lazima ionwe kwa jicho la tatu kutokana na jiografia yake hususani katika suala la watumishi, dawa na vifaa tiba.

“Haiwezekani kuona wananchi wanatumia gharama kubwa ya Sh 250,000  ya kupanda ndege kwa ajili ya kufuata kipimo cha typhoid Dar es Salaam, Katibu Tawala nakuomba ushirikiane na timu yako kutatua jambo hili kwa haraka,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles