SERIKALI imesema inakamilisha utaratibu mpya wa kuwaruhusu wakulima kuanza kuuza chakula nje ya nchi.
Akitoa kauli ya Serikali bungeni jana, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba, alisema utaratibu huo utakamilika ndani ya wiki moja kuanzia jana.
Dk. Tizeba alitoa taarifa hiyo baada ya mwanzoni mwa wiki, wabunge wawili wa CCM, Joseph Msukuma wa Geita Vijijini na Ally Kessy Mohamed wa Nkasi Kaskazini, kuomba mwongozo wakitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kunusuru mazao ya chakula yanayoharibika kutokana na Serikali kuzuia mauzo ya chakula nje ya nchi.
Katika maelezo yake jana, Dk. Tizeba, alisema wizara yake kwa sasa ndiyo yenye dhamana ya kutoa vibali vya kuuza na kuingiza mazao ya chakula kwenda na kutoka nje ya nchi.
“Kwa hiyo wizara inakamilisha utaratibu mpya wa kuuza chakula nje ya nchi ndani ya wiki moja kuanzia sasa na vibali kwa mazao aina ya mahindi na mchele, vitaendelea kutolewa,” alisema Dk. Tizeba.
Kuhusu upatikanaji wa chakula nchini, Dk. Tizeba, aliwatoa hofu Watanzania na kusema kuna chakula cha kutosha kwa asilimia 123.
“Mwaka huu, Serikali imefanya tathmini ya uzalishaji wa mazao ya chakula kwa mwaka 2015/2016 na upatikanaji wa chakula kwa mwaka 2016/2017.
“Tathmini hiyo ilionyesha uzalishaji wa chakula kitaifa utafikia tani 16,172,841 wakati ili nchi ijitosheleze kwa chakula mwaka huu wa 2016/2017, tunahitaji tani 13,159,326.
“Kulingana na takwimu hizo, nchi itakuwa na chakula cha kutosha chenye ziada ya asilimia 123,” alisema Dk. Tizeba.
Kuhusu ununuzi wa chakula hicho kwa wakulima, alisema wakala wa chakula umepeleka katika kanda zake Sh bilioni 27.7 kwa kuwa lengo ni kununua tani 100,000 za nafaka.
Pia alisema wakala umeomba serikalini Sh bilioni 69.5 kwa ajili ya kununua nyongeza ya tani 100,000 za chakula.
Katika hatua nyingine, Dk. Tizeba, alisema hivi sasa wizara yake iko katika hatua za mwisho za kuanzisha Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko itakayokuwa na mamlaka ya kutoa vibali na kudhibiti ubora, viwango na bei za mazao ya nafaka mchanganyiko.