27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Tanzania itapata sheria ya namna gani ya haki ya kupata taarifa?

Mwakyembe akiteta jambo na Rais John MagufuliNa DEUS KIBAMBA

BUNGE limeanza vikao vyake vya mkutano wa nne wa Bunge la 11 mjini Dodoma. Kwetu sisi wafuatiliaji wa masuala ya kibunge, kijamii na kisiasa, tunafahamu fika mkutano huu ni mahususi kwa ajili ya kusomwa kwa miswada mbalimbali.

Miongoni mwa miswada inayotarajiwa kusomwa katika vikao hivyo ni wa Sheria ya Haki ya Kupata Taarifa wa mwaka 2016, ambao unakuwa unasomwa kwa mara ya pili.

Muswada huu sasa umefikia hatua nzuri baada ya kukwama kwa miaka takribani kumi tangu Wizara ya Habari ilipouchapisha kwa mara ya kwanza mwaka 2006.

Kusema ukweli, muswada huu ni moja kati ya miswada iliyoleta vuta nikuvute kwa muda mrefu kuliko mwingine wowote uliowahi kutokea katika historia ya miswada ndani ya nchi yetu.

Tayari Kamati ya Bunge ya Masuala ya Katiba, Sheria na Utawala imekutana na wadau wiki iliyopita katika kujaribu kupata maoni ya dakika za lala salama kabla ya Waziri hajaenda kuuwasilisha muswada huo bungeni kwa mara ya pili.

Mwanzoni, muswada huu kusomwa katika hali yake ya sasa ilikuwa ni kwenye mkutano wa tatu wa Bunge la Bajeti kati ya Aprili na Julai mwaka huu.

Moja ya taasisi zilizofika mbele ya kamati kutoa maoni ya mwisho katika kuunakshi muswada huu kabla ya kuwasilishwa bungeni ni Kituo cha Taarifa kwa Wananchi na Jukwaa la Katiba Tanzania ambao walifika mbele ya kamati chini ya mwamvuli wa mashirika yanayotetea uhuru wa habari, haki ya kupata taarifa na uhuru wa kuwa na maoni na kujieleza uitwao CORI chini ya uratibu wa Baraza la Habari Tanzania.

Kama inavyoelezwa katika malengo, madhumuni na sababu za muswada wenyewe, lengo kuu la kuhitajika kwa sheria hii ni kupanua wigo wa uombaji, utoaji na usambazaji wa taarifa zilizo katika mikono ya taasisi za umma na binafsi kutoa taarifa ama kwa hiari yao (proactively) au kutokana na maombi yanayofanywa.

Wakati taarifa zinazopaswa kutolewa na taasisi za umma na idara za serikali ni zile zote zilizo katika himaya ya mikono yao isipokuwa zilizo na kinga ya kisheria, taasisi binafsi zina wajibu wa kutoa taarifa ambazo zina masilahi fulani kwa umma zaidi ya masilahi kwa mtu mmoja, kikundi au shirika fulani. Huu ndio utendaji wa kimataifa kuhusu sheria hizi.

Kwa sababu ya malengo ya muswada yanayobainishwa katika muswada na kutokana na ibara za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambazo zinalenga kuleta utekelezaji wake, jina la muswada limekwepa uhalisia wa kwanini sheria inatungwa.

Kwa maoni yangu, jina halisi la muswada huu linapaswa kuwa Muswada wa Sheria ya Haki ya Kupata Taarifa, 2016. Dhana hapa inapaswa kuwa taarifa ni haki ya kila mtu kuomba, kupatiwa na kusambaza ikiwemo kuchapisha popote bila kujali uraia wake wala mipaka ya nchi.

Aidha, inapaswa ijulikane wazi kuwa mtu kwa tafsiri ya kisheria atakuwa na maana zake mbili, yaani mtu kama binadamu na mtu wa kisheria ambaye ni taasisi, shirika au kampuni. Katika dunia ya sasa, uzoefu unaonesha kuwa maombi ya taarifa kutoka mashirika ndiyo mengi kuliko maombi ya watu binafsi.

Pamoja na yote hayo, kuna suala la tarehe ya kuanza kutumika kwa sheria.  Kwa sheria iliyosubiriwa na kubishaniwa kwa miaka mingi kama hii, kusema kwamba tarehe ya kuanza kutumika kwake itategemea hiari ya waziri husika ni kuweka uwezekano wa kuchelewesha matumizi zaidi na zaidi. Badala yake, inapendekezwa kuwa tarehe ya kuanza kutumika kwa sheria baada ya kupitishwa na Bunge, itamkwe bayana katika sheria yenyewe. Uzoefu wa kimataifa na wetu wenyewe hapa nchini unaonesha kuwa zipo sheria zilizowahi kutungwa na Bunge na zikakaa zaidi ya miaka kumi bila kuanza kutumika kwa sababu tu waziri mwenye dhamana ya sheria hiyo hajaamua kupangia tarehe ya kuanza matumizi ya sheria hiyo.

Pia, mawaziri wengi wamekuwa wakigwaya kazi ya utengenezaji kanuni za sheria na kuzidi kuchelewa kutangaza tarehe ya matumizi kwa sababu tu ya kanuni kutokuwa tayari. Pendekezo hapa ni kuweka katika sheria lugha inayosema sheria itaanza kutumika siku kadhaa baada ya kupitishwa na Bunge na kupata saini ya rais. Kimataifa, siku tisini ni muda mzuri wa kutosha na kwa sababu hiyo sheria hii inaweza kutangazwa Januari mosi, 2017 kama tarehe rasmi ya kutumika sheria hiyo.

Utaratibu huu umewahi kutumika hapa nchini kwa sheria kadhaa ikiwemo ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ilipangiwa Desemba mosi, 2011 kama siku ambayo sheria hiyo ingeanza kutumika rasmi.

Sheria pia imetumia maneno mengi yenye uwezekano wa kuzua utata katika matumizi na ambayo yanahitaji tafsiri. Kwa mfano, maneno kama masilahi ya umma, kibiashara, kiuchumi, taarifa za kupotosha na mengine ya namna hiyo ni vema yakapatiwa tafsiri katika sheria hii kuliko kutegemea tafsiri ya sheria ambayo inaweza kutoa maana kwa mazingira tofauti na mazingira ya sheria hii kwa sababu ya upya wake.

Kwa tafsiri yetu, masilahi ya umma imaanishe nia au lengo ambamo manufaa yake ni kwa ajili ya watu wengi ikilinganishwa na mtu mmoja, kikundi au taasisi fulani. Masilahi ya umma itakuwa ni pale ambapo faida za kutoa taarifa fulani zinakwenda kwa watu wengi zaidi kuliko kuzuia kutoa taarifa.

Kwa bahati nzuri, tafsiri hii ya masilahi ya umma ninayoipendekeza inafanana sana na iliyowahi kutolewa na Mahakama ya Rufani ya Tanzania katika shauri mbele yake kwenye kesi Na. 30 ya mwaka 2004 ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya Sisi Enterprises.

Mwisho, sheria hii ina mgongano mkubwa katika kutoa adhabu kwa makosa yatakayotendwa chini yake. Wakati sheria ikishindwa kumwadhibu ofisa tarafa anayekataa kutoa taarifa zilizoombwa bila sababu za msingi, sheria hiyo hiyo inaweka adhabu kubwa mno kwa mtu yeyote anayetoa taarifa iliyo na zuio la kisheria chini ya kifungu cha 6 (6) ambapo anaweza kufungwa kwa kipindi cha miaka kati ya 15 na 20 pasipo hata mbadala wa adhabu hii.

Adhabu hii ni kubwa mno kwa kosa hilo kiasi cha kukaribia kosa la kuua.

Ni wazo langu kuwa sheria itumie lugha ya adhabu isiyozidi badala ya kutumia maneno yasiyopungua. Pia, ninashauri adhabu ya kifungo cha miaka isiyozidi mitano au faini isiyozidi milioni tano.

Vinginevyo, makosa yenyewe pia yatazamwe upya. Kwa mfano, hivi kweli itakuwa ni kosa kwa mtu kutoa taarifa zote zinazohusu mambo ya nje katika nchi yetu? Je, mambo yote ya nje ni ya kiusalama? Kwa maono yangu, kifungu cha 6 (2) d cha muswada kinajumuisha taarifa za Mambo ya Nje ya Nchi kama taarifa za kiusalama kimakosa kwa kuwa yapo mambo mengi ya nje ambayo si ya kiusalama na hayapaswi kuwekewa zuio la pamoja kama ilivyowekwa na muswada huu wa sheria. Sheria pia inapaswa kufanywa kuwa na ukuu juu ya nyinginezo zote kuhusu haki ya kupata taarifa ili panapotokea mgongano kati ya sheria moja au mbili dhidi ya sheria hii ya Haki ya Kupata Taarifa, iwe bayana kuwa sheria hii ndiyo itatanabahi.

Kuhusu masuala mengine ya msingi, nayaona maeneo matatu yanayohitaji maboresho. Kwanza, kifungu cha 21 kinafanya makosa kwa kuruhusu mtoa taarifa kutoza ada kwa taarifa anayoitoa. Duniani kote, taarifa ni haki wezeshi kwa kila mtu kwa kuwa mtu akikosa taarifa anaweza kukosa haki zote za msingi.

Hivyo basi, taarifa inapaswa kutolewa bure kwa watu wote bila malipo isipokuwa kunapokuwa na uhitaji wa kudurufu. Aidha, kunapaswa kuwa na haki kwa mtu anayenyimwa taarifa kuweza kukata rufaa kwa chombo huru kitakachotenda haki. Namna ambavyo rufaa imewekwa katika kifungu cha 19 (3) inachekesha.

Kwamba mtu akiomba taarifa na kukataliwa na ofisa taarifa, basi anaweza kukata rufaa kwa mkuu wa taasisi ya mtoa taarifa ni kama kesi ya ‘ngedere’ kukabidhiwa kwa ‘nyani’.

Vivyo hivyo, kusema kuwa endapo mtu huyo hataridhishwa na uamuzi wa mkuu wa taasisi, basi atakata rufaa kwa waziri husika nikitarajia yasiyowezekana kwa kuwa mara nyingi au zote, waziri atapenda kutotofautiana na mkuu wa taasisi aliyetoa maamuzi ya malalamiko ya awali.

Na kwamba maamuzi ya waziri yatakuwa ni ya mwisho, ni kuminya haki ya mtu kupeleka shauri mahakamani kwa jambo lolote ambalo limemkera kutokana na maamuzi ya chombo chochote kile.

Ni mapendekezo yangu kuwa kipindi kilichowekwa chini ya kifungu cha 11 (1), kwa ofisi yenye taarifa kuitoa au hata kujibu maombi ikiwemo kukiri kupokea maombi hayo ni kirefu mno. Kwamba maombi yajibiwe katika siku 30 hata kwa kusema tumepokea maombi yako ni kukiuka utendaji uliokwishaanzishwa hivi sasa chini ya mikataba ya huduma kwa wateja na miongozo ya Serikali za mitaa.

Kwa ushauri wangu, siku tatu za kazi zinatosha kukiri kupokea maombi ya taarifa, ambapo siku saba nyingine ofisa taarifa awe amejibu kama taarifa husika itapatikana au iko katika ofisi nyingine ambapo atahamishia maombi hayo kwa taasisi hiyo nyingine. Muda wa mwisho kabisa katika kushughulikia maombi ya taarifa hadi kutoa taarifa nyenyewe unapaswa usizidi siku kumi na nne.

Ni matumaini yangu kuwa mawazo haya yatasaidia kuboresha Muswada wa Sheria ya Haki ya Kupata Taarifa wa Mwaka 2016, ili uzae sheria nzuri ya mfano katika ukanda huu wa Afrika.

Muswada huu tayari una hali nzuri zaidi ikilinganishwa na rasimu yake ya awali mnamo mwaka 2006. Kila la kheri kwa watunga Sheria wetu mjini Dodoma kuanzia wiki hii.

Deus Kibamba ni Mhadhiri wa Msuala ya Uhusiano wa Kimataifa jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya JUKWAA LA KATIBA TANZANIA. Pia, ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo Cha Taarifa kwa Wananchi (TCIB) kinachoendesha vituo vya taarifa kwa wananchi kote nchini. Aidha, ni mjumbe wa Jopo la Washauri na Watetezi wa Haki ya Kupata Taarifa linaloratibiwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) tangu mwaka 2006. Anapatikana kwa nambari ya simu: +255 788 758581

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles