NA FLORENCE SANAWA, LINDI
MKUU wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi, amejikuta akitumia Jeshi la Polisi kukusanya wananchi ili wafanye usafi katika maeneo yao hususani barabarani.
Hatua hiyo imesababisha foleni isiyo ya lazima kwa zaidi ya saa nzima kwa mabasi yaendayo Dar es Salaam na malori ya mizigo.
Akizungumza na wananchi wa eneo hilo mara baada ya kumaliza usafi, alisema eneo hilo limekuwa chafu na kuhatarisha afya za wakazi wa eneo hilo.
“Tumelazimika kutumia Jeshi la Polisi ili kuhakikisha wananchi wanajitolea kufanya usafi bila kulazimishwa,” alisema.
Zambi alisema suala la usafi litakuwa endelevu kila Jumamosi ili kuhakikisha mkoa unakuwa msafi kwa kuepukana na magonjwa ya mlipuko hasa kipindupindu sambamba na kujenga makaro kwa ajili ya kutunzia takataka.
“Hivi inawezekanaje tunakuwa na ofisi ya kata, tumechaguliwa na wananchi wengine wameajiriwa na Serikali, hawana vyoo wanakwenda kujisaidia kwenye majumba ya watu, hatuwezi kwenda kwa kasi hiyo, wale wasioweza kwenda na kasi ya awamu hii, hawana nafasi tena katika Serikali hii,” alisema.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Pangatena, Bakari Ding’unde, alisema usafi huo umekuwa chachu kwao na kuushukuru ugeni huo ambao umeongeza hamasa ya usafi kwa wananchi wa eneo hilo.