Na ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM
WAUZA bidhaa wanaomzunguka kocha wa zamani wa timu ya Manchester United, Sir Alex Ferguson, wameanza kuweka ujumbe mpya wa maneno katika vitambaa vya shingoni vya timu hiyo tangu ilipocheza mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Engalnd, uliochezwa uwanja wa Old Trafford.
Zlatan Ibrahimovic na Paul Pogba, wanaweza kuwa kinyume na matarajio katika kazi yao lakini wakawakilisha vema sura mpya ya klabu hiyo maarufu duniani.
United walifanya usajili mkubwa wa wachezaji wao mapema, lakini haikutosha waliamua kuingia tena sokoni kwa kufanya usajili wa gharama na wa kihistoria ukimjumuisha mshambuliaji wa nafasi ya tatu kwa ubora katika ulimwengu wa soka, Ibrahimovic.
Maandalizi hayo yalikuwa kwa ajili ya kuanza kwa msimu mpya kwa mafanikio chini ya kocha mpya wa timu hiyo, Jose Mourinho, ambaye tayari ameanza kuonesha makali yake.
Kabla ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya timu ya Southampton hivi karibuni, United waliwahi kufungwa msimu uliopita na timu hiyo wakiwa katika uwanja wa Old Trafford.
Lakini mambo yameanza kubadilika katika uwanja huo ukiwa chini ya utawala wa fikra pevu za Mourinho mwenye rekodi nzuri ya kushinda michezo yake ya nyumbani.
Uwanja wa Old Trafford umerudi katika msisimko wake tena kama ambavyo awali ulivyokuwa na heshima na kuonekana sehemu ya adhabu kwa timu pinzani.
Wachezaji mbalimbali mahiri na hodari wamecheza katika uwanja huo kifalme, lakini King Zlatan na Prince Pogba, huenda wakawa watawala wakubwa na kufuta kabisa utawala wa waliopita.
Huo ndio ukweli halisi bila shaka, Pogba aliyerejea katika klabu hiyo baada ya kuondoka mwaka 2012, anatarajiwa kufanya vema katika muda wote atakaokuwa na timu hiyo.
Nyota huyo amekuja kunogesha eneo la ushambuliaji linaloongozwa na King Zlatan, kwa kutoa ushirikiano wa pasi murua akiwa sambamba na mkongwe na nahodha wa timu hiyo, Wayne Rooney.
King Zlatan hana muda wa kupoteza ambao wengine wanaamini kwamba alitakiwa azoee mazingira ndipo afanye vizuri katika mazingira mapya ya timu hiyo na ligi hiyo kwa ujumla.
Kwani nyota huyo anaamini juu ya vipimo vya bao alivyotumia akiwa katika timu ya Paris Saint-Germain (PSG) ndivyo vitatosha kuvitumia katika michezo ya Ligi Kuu England.
Uwezo na nguvu aliyonayo katika kupiga mipira ya vichwa ndiyo iliyomchanganya hata beki wa Southampton, Jose Fonte na kumruhusu kuiandikia United bao la kuongoza kabla ya bao la pili la penalti lililofungwa na Ibrahimovic pia.
Hakuna shaka yoyote kwa sasa katika chumba cha kubadilishia nguo mbele ya Rooney akiwa na King Zlatan.
King Zlatan awali alikuwa katika klabu hiyo kifikra akitarajia mafanikio makubwa atakapojiunga nayo hata hivyo ujio wake na Prince Pogba umechochea matumaini ya furaha katika timu hiyo.
Prince Pogba alitumia muda mwingi zaidi kucheza mpira wa kikapu akiwa na Romelu Lukaku badala ya mpira wa miguu kitendo hiki alikifanya kwa sababu alikuwa akitafuta kitu cha kumstarehesha na kumpa imani.
Bado kuna hisia kwamba nyota huyo hana miguu inayofanana na aina ya kiungo bora na ghali kama ambavyo anadhaniwa kwa kuwa hana uwezo wa utulivu wa utawala ndani ya uwanja kwa muda wa dakika 90.
Hata hivyo, uwepo wake dhahiri ni msisimko wa kweli kwa ajili ya mashabiki wa timu ya Manchester United msimu huu.
Mchanganyiko wa aina tofauti ya wachezaji na kutengeneza ukamilifu kwa kuwatumia mchezaji kama Eric Bailly ni wazi kwamba Pogba kazi yake itakuwa si ya kutumia nguvu nyingi kupata mafanikio.
Kwa kuwa atakuwa katika uongozi thabiti wa Ibrahimovic na Henrikh Mkhitaryan ambaye anaonekana kufanya vizuri zaidi chini ya Mourinho.
Klabu hiyo imeongeza thamani ya wachezaji wake katika soko la usajili ikiwa chini ya kocha huyo ambaye ni mshindi mara mbili wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Msimu huu unaweza kuwa wa mafanikio zaidi kwa klabu hiyo inayoshiriki Ligi ya Europa.
Imejitahidi kuwashawishi wachezaji wenye majina makubwa kujiunga nao ili kutafuta mafanikio yaliyopotea muda mrefu.
Kila mmoja anatamani kuangalia michezo ambayo itakuwa inapigwa kwenye uwanja wa Old Trafford, huku United ikiwa mbele ya mashabiki wao.