WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amesema anasikitishwa na siasa chafu zinazoanza kufanywa dhidi yake.
Amesema mikakati ya baadhi ya watu kutaka kumhusisha na imani za kidini kwa lengo la kumgombanisha, kamwe hazina nafasi mbele za Mungu.
Katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana, Waziri Nyalandu alisema kamwe hajawahi na hatarajii kudharau wala kubagua imani ya dini nyingine.
“Nimesikitishwa na kuumizwa na taarifa ambazo hazina mashiko za uzushi na za kutunga zenye lengo la kunipaka matope kwa kunihusisha na maneno ambayo kinywa changu hakikuyatamka wala kuyafanyia rejea.
“Katika maisha yangu kama Mtanzania, kama kiongozi na kama Mkristo, sijawahi kutoa kauli hasi dhidi ya imani za dini nyingine ikiwamo dini ya Kiislamu,” ilisema taarifa hiyo.
Kauli ya Waziri Nyalandu, imetokana na taarifa zenye lengo la kumgombanisha na viongozi na waumini wa dini ya Kiislamu zilizosambazwa juzi kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Taarifa hiyo ilisema siku ya mkesha wa mwaka mpya Desemba 31, mwaka jana, katika ibada ya iliyofanyika kwenye Kanisa la Ephata lililopo Kibaha mkoani Pwani, Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Ephata, Josephati Mwingira, anadaiwa kutoa kauli zenye mwelekeo wa kukashifu Uislamu.
Taarifa hizo zimedai kuwa, Mchungaji Mwingira alisema mwisho wa utawala wa majini na mapepo umefika, kauli ambayo taarifa hizo zimedai kuwa Nyalandu hakuikemea licha ya kuwapo kanisani hapo.
Nyalandu katika taarifa yake, alisema kitendo cha kumhusisha na madai ya kauli hizo, si sahihi na ni kumwekea maneno kinywani.
Alisema amekuwa mstari wa mbele kushirikiana na watu wa dini na itikadi zote na kwamba, hivi karibuni atazuru Saudi Arabia kwa mwaliko wa mwana Mfalme wa nchi hiyo.
“Hizi ni fitna zenye lengo la kupakana matope kwa misingi ya ubaguzi wa kidini, nimeshiriki kupeleka masheikh katika jimbo langu kwenda kuhiji Macca, mpango ambao umekuwa endelevu kwa miaka zaidi ya 10 sasa.
“Ni muhimu demokrasia ikaendelezwa kwa kuhimiza mijadala ya kuwaletea wananchi maendeleo na sio kwa kueneza chuki za kidini, kijinsia, au kikabila,” alisema.