MILWAUKEE, MAREKANI
MGOMBEA urais wa Marekani kupitia Chama cha Republican, Donald Trump amesema ushahidi wa awali unaonyesha ilikuwa halali kwa kijana mweusi kuuawa na polisi mjini hapa Jumamosi iliyopita.
Mauaji ya kijana huyo, Syville Smith katika mji huu wenye Wamarekani wengi weusi yalisababisha maandamano makubwa hivi karibuni.
Katika kampeni hiyo Trump alimshambulia mpinzani wake Hilary Clinton kwamba amechangia kuwepo kwa vurugu katika mji huo.
“Utekelezaji wa sheria, kujumuisha jamii, utendaji bora wa polisi ni mambo ambayo nchi yetu inahitaji. Lakini mpinzani wangu hawajali watu wa hali ya chini, alikuwa anawapinga polisi, hivyo basi mniamini mimi kwa sababu mwenzangu huyu anahamasisha uhalifu,” alidai.
“Vitendo vinavyohamasisha ubaguzi kwenye jamii yetu ni mambo ambayo yamekuwa yakichochewa na mpinzani wangu ambaye ameshiriki moja kwa moja vurugu za Milwaukee na maeneo mengine katika nchi yetu,” alisema.
Wakati huo huo, mgombea wa urais kwa tiketi ya chama cha Republican Donald Trump ameifanyia mabadiliko timu yake ya kampeni kwa mara ya pili kipindi cha miezi miwili akiteua meneja mpya na afisa mkuu.
Umaarufu wa Trump umeonekana kushuka tangu mkutano wa chama hicho uliofanyika mwezi uliopita.