Jeshi la Sudan Kusini, waasi kuunganishwa

Taban Deng Gai
 Taban Deng Gai
Taban Deng Gai

NAIROBI, KENYA

SERIKALI ya Sudan Kusini imesema italiunganisha jeshi la nchi hiyo pamoja na vikosi vya waasi ifikapo Mei 2017.

Akitoa tangazo hilo mjini hapa jana, Naibu wa Kwanza wa Rais, Taban Deng Gai pia alimlaumu aliyekuwa Makamu wa Rais, Riek Machar kwa kuhujumu mkataba wa amani uliotiwa saini baina yake na Rais, Salva Kiir.

Gai alidai kiongozi huyo wa waasi alikuwa akiongoza serikali nyingine sambamba na Kiir mjini Juba kabla hajakimbia kufuatia machafuko yaliyoibuka katika mji huo mkuu wa Sudan Kusini.

“Ni rahisi kwetu kwa sasa kuanza utekelezaji wa makubaliano ya amani kwa sababu tuna utulivu. Wakati Riek Machar alipokuwa Juba, suala la majeshi mawili lilikuwa tatizo. Sasa tunaelekea haraka kupata jeshi moja la taifa ifikapo Mei mwaka ujao,” alisema.

Alisema yeye na wengineo waligoma kukubaliana na Machar wakati alipowashawishi waondoke naye kutoka Juba mwezi uliopita.

“Alitutaka tuondoke naye, lakini tulisema hapana, kwa sababu hatuko tayari kuendekeza matendo yanayokwamisha amani katika nchi yetu. Ninapaswa kuleta amani katika serikali na nchi yetu na hivyo tunasonga mbele,” alisema.

“Iwapo ataamua kurudi, tutajadili, lakini anajua safari hii anapaswa kuwasikiliza vijana wake,” alisema.

Alisema Sudan Kusini bado inasubiri viongozi wa kikanda kukutana mjini Juba kujadili upelekaji wa kikosi cha askari wa kulinda amani kama ilivyopitishwa na Baraza la Usalama wa Umoja wa Mataifa.

Gai alisema alishakutana na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta kumweleza maendeleo ya makubaliano ya amani na kuomba msaada wa kuijenga upya Sudan Kusini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here