Asifiwe George na Elias Saimon(TUDARCO), Dar es Salaam
MBUNGE wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema) amehojiwa na polisi kwa saa tatu akituhumiwa kuandika makala iliyochapishwa kwenye gazeti la Mwanahalisi la Julai 25 hadi 30, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, v Hezron Gyimbi, alisema mbunge huyo alihojiwa kutokana na kauli b anazozitoa katika magazeti yake.
Alisema maneno hayo ya Kubenea yanaweza kuleta uchochezi na uvunjifu wa amani.
“Kutokana na kauli zake anazozitoa mara kwa mara zenye viashiria vya uchochezi ndiyo maana tumemhoji na tumemuachia kwa dhamana lakini kesho asubuhi (leo) atatakiwa kuripoti tena kuendelea na mahojiano,” alisema Gyimbi.
Mbunge huyo wa Ubungo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Hali Halisi ambao ni wachapishaji wa gazeti la Mwanahalisi, Mseto lililofungiwa kwa miezi 36 na Mawio ambalo limefungwa kwa muda usiojulikana, aliwasili kituoni hapo jana saa 7.00 mchana akiwa na gari namba T 216 BHH Land Cruiser akiwa ameongozana na wanasheria wake, Tundu Lissu na Fredrick Kihwelo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Lissu alisema mteja wake alihojiwa na polisi kuhusu makala aliyoiandika katika gazeti lake wiki tatu zilizopita ikielezea hali ya ukiukwaji wa haki za binadamu Visiwani Zanzibar.
“Kwa mujibu wa polisi makala hiyo ni ya uchochezi na polisi walikuwa wakiuliza maswali yao ya ajabu ajabu na aliulizwa kwamba alijaribu kuonana na polisi kuhusiana na hiyo makala yake.
“Kwa kiasi kikubwa alihojiwa maswali ambayo majibu yake yote yapo kwenye hiyo makala yenyewe,” alisema Lissu.