Na MWANDISHI WETU, ZANZIBAR
KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amekataa kusalimiana kwa kushikana mkono na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.
Tukio hilo lilitokea jana mchana wakati wa mazishi ya Rais wa pili wa Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi, aliyezikwa jana katika makaburi yaliyoko maeneo ya Migombani visiwani hapa.
Katika Uchaguzi Mkuu mwaka jana, Maalim Seif alishindana Dk. Shein ambaye aliibuka mshindi katika uchaguzi wa marudio wa Machi 20, mwaka huu.
Hata hivyo, Maalim Seif alilalamikia ushindi wa Dk. Shein kwa kile alichosema haukuwa halali kwa kuwa alifanyiwa hujuma na kuporwa ushindi wake uliopatikana Oktoba 25 mwaka jana.
Mazishi ya marehemu Jumbe yalifanyika jana saa saba mchana kisiwani Unguja, ambapo Dk. Shein aliwaongoza mamia ya watu waliofika msibani hapo.
Wakati akiwa makaburini, Dk. Shein alisalimiana na waombolezaji mbalimbali kwa kuwashika mikono, lakini alipopeleka mkono kwa Maalim Seif, mwanasiasa huyo mkongwe aliukataa mkono huo na kuwashangaza waombolezaji.
Msiba huo ulihudhuriwa na viongozi na watu mbalimbali wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja Serikali ya Zanzibar.
Viongozi waliohudhuria ni pamoja na marais wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwamo Benjamin Mkapa na Ali Hassan Mwinyi.
Mbali na hao, pia alikuwapo Makamu wa Rais mstaafu, Dk. Mohammed Gharib Bilal, Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa na Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume.
Wengine ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na aliyekuwa Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Habib Ali Kombo.
Akisoma risala kwa niaba ya Serikali zote mbili, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohammed Aboud Mohammed, alisema kifo cha Jumbe ni pigo kwa Watanzania.
“Enzi za uhai wake, mzee Jumbe alifanikiwa kuazisha mfumo wa kuandikwa kwa Katiba ya Zanzibar pamoja na kuwakusanya wanasheria na kutaka nchi kuendeshwa kwa mujibu wa sheria,” alisema.
Aboud alisema Serikali kwa kushirikiana na familia ya marehemu, wametekeleza wosia ulioachwa na marehemu, aliyesema siku akifariki asipigiwe mizinga na asizikwe kijeshi.
“Tumefanya mazishi haya kwa kutekeleza yale marehemu aliyoyaandika na Serikali imeshirikiana kikamilifu na watoto wake ili kuhakikisha yale yote aliyoyausia ndio tunayatekeleza.
“Tunashukuru tumekwenda vizuri tokea mwanzo hadi mwisho bila ya misukosuko yoyote,” aliongeza Aboud.
Katika mazishi hayo hakukuwapo na mizinga kama yanavyofanyika mazishi mengine ya viongozi wakuu wa Serikali na jeneza lake lilibebwa kwa kufunikwa kitambaa cha kawaida na si bendera ya taifa wala ya chama.
Wakati huo huo, Lowassa alipokuwa akimzungumzia marehemu Jumbe, alisema Watanzania wamepata pigo kwa kuondokewa na kiongozi ambaye alikuwa anajiamini.
“Watanzania tunatakiwa tujifunze kujiamini kutoka kwa marehemu wetu huyu kwani alikuwa tayari kwa lolote katika mambo yake anayoyataka katika uongozi wake.
“Ujasiri aliokuwa nao marehemu Alhaji Jumbe ni wa kipekee, kwa hiyo Watanzania wanapaswa kumkumbuka kwa ushupavu wake,” alisema Lowassa.
Naye Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, alisema Tanzania imepoteza mwandishi wa siasa kwani enzi za uhai wake aliandika vitabu vingi vyenye mwelekeo wa siasa.
“Watanzania hatuna utaratibu wa kusoma vitabu, lakini nakuombeni tuvisome vitabu vya Alihaji Jumbe ili tuweze kujifunza kutoka kwake.
“Umahiri aliokuwanao katika kuandika vitabu vyake hasa vile vya kisiasa ni nguzo kwa uongozi wa Tanzania na wananchi kama watavisoma na kuvifanyia kazi,” alisema.