29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Mastaa wa muziki Afrika waliosaini lebo za kimataifa

Tiwa Savage
Tiwa Savage

NA BADI MCHOMOLO,

NI wazi kwamba muziki wa barani Afrika kwa sasa unazidi kupasua anga na kusogea nje ya bara hili kutokana na jitihada na malengo ambayo wamejiwekea.

Kwa sasa kuna wasanii kutoka Afrika ambao wanafanya vizuri Ulaya na kukubalika zaidi tofauti na ambavyo wanakubalika baadhi ya sehemu za Afrika.

Kwa kuliona hilo makampuni makubwa ya muziki barani Ulaya yameanza kufanya kazi na wasanii wa Afrika kwa kuwapa mikataba minono ambayo inaweza kuwafanya wawe zaidi ya walivyo sasa.

Hapa tumekutayarishia listi ya wasanii kutoka bara la Afrika ambao wamesaini mikataba na makampuni makubwa ya muziki huko Ulaya.

GLORIA MECHEO

Huyu ni rapa kwa upande wa wanawake kutoka nchini Kenya, amekuwa na jina kubwa kutokana na uwezo wake wa kufanya muziki wa rap, kutokana na kazi hiyo ya muziki msanii huyo amekuwa akijulikana kwa jina la Xtatic.

Rapa huyo amefanikiwa kuingia mkataba na Kampuni ya Sony Music Entertainment Africa, ambayo ni tawi la Kampuni ya Sony inayosimamia wasanii mbalimbali duniani.

Hata hivyo Xtatic, baada ya kusaini dili hilo, amedai maisha yake yameanza kubadilika kwa kiasi kikubwa kwa kuwa kila anachotaka kukifanya katika muziki lazima Sony wasimamie, hivyo anapata manufaa makubwa.

ALI KIBA

Huyu ni msanii wa muziki wa Bongo Fleva, kutoka hapa home –  Tanzania, anajulikana kwa jina la ‘King Kiba’ amekuwa akifanya vizuri katika muziki wake na kuifanya kampuni ya muziki ya Sony kukaa mezani na msanii huyo na kusaini mkataba.

Kwa sasa msanii huyo anafanya kazi zake za muziki huku akisimamiwa na kampuni hiyo kubwa duniani. Mkataba huo ulisainiwa Mei, mwaka huu nchini Afrika Kusini.

Baada ya kusaini mkataba huo King Kiba, alidai kwamba huu ni wakati wake wa kuzidi kupaisha sauti yake ndani na nje ya Afrika kwa kuwa amepata wasimamizi wa uhakika wa kazi hizo.

TIWA SAVAGE

Ni nyota wa muziki kutoka Nigeria, amekuwa akifanya vizuri na ushindani mkubwa kwa wasanii wa kike nchini humo, uwezo wake ulimfanya avuke mipaka na kukubalika na wasanii wakubwa nchini Marekani.

Kutokana na uwezo wa msanii huyo, rapa Jay Z ambaye anayemiliki Kampuni ya Roc Nation ameamua kumsainisha mkataba wa pesa ndefu na kufanya naye kazi.

Wasanii wengine wanaofanya kazi na kampuni hiyo ni pamoja na J. Cole,  Big Sean, Rihanna, Kanye West, Grimes, Demi Lovato, DJ Khaled, T.I. Rita Ora na wengine wengi.

DAVIDO

Ni staa wa muziki nchini Nigeria, muziki wake kwa sasa unazidi kuvuka mipaka, kampuni kubwa ambayo inasimamia muziki nchini Marekani, HKN Records, ilikaa mezani na msanii huyo kisha kumsainisha mkataba wa kusimamia kazi zake.

Kutokana na mkataba huo, msanii huyo kwa sasa amekuwa akifanya kazi na wasanii mbalimbali nchini Marekani na amekuwa akiwania tuzo mbalimbali za muziki duniani kama vile BET, MTV, hivyo ni kutokana na usimamizi bora wa kampuni hiyo.

A.K.A

Nyota wa muziki nchini Afrika Kusini, anafanya vizuri kwa sasa na aliwania tuzo katika BET mwaka huu nchini Marekani, jina lake kamili ni Kiernan Jarryd Forbes, alisaini mkataba na kampuni ya Sony tangu mwaka 2014 mpaka sasa anaendelea nao.

VICTORIA KIMANI

Ni mkali wa muziki kutoka nchini Kenya, amefanya vizuri na anaendelea kufanya vizuri ndani na nje ya Kenya. Kampuni ya kusimamia kazi za muziki nchini Nigeria ambayo inajulikana kwa jina la Chocolate City, ilisaini mkataba na msanii huyo kwa ajili ya kusimamia kazi zake.

Mbali na msanii huyo kuna wasanii wengine ambao wanasimamiwa na kampuni hiyo kama Jude Abaga ‘M.I’ Panshak Zamani ‘Ice Prince’ na Olawale Ashimi ‘Brymo’ wote kutoka nchini Nigeria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles