29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Waliofukuzwa polisi wakamatwa kwa ujambazi

Wilbrod Mutafungwa
Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbrod Mutafungwa

 

Na UPENDO MOSHA – MOSHI

JESHI la Polisi mkoani Kilimanjaro, linawashikilia watu 15 kwa tuhuma za uhalifu na unyang’anyi wa kutumia silaha, wakiwamo wawili waliokuwa askari polisi.

Taarifa hiyo ilitolewa jana kwa vyombo vya habari na Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbrod Mutafungwa.

Kwa mujibu wa kamanda huyo, watuhumiwa hao walikamatwa na askari polisi kwa nyakati tofauti katika maeneo mbalimbali mkoani hapa.

“Baada ya kuendesha msako, tulifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao, wakiwamo wawili waliokuwa askari polisi zamani.

“Wale waliokuwa askari polisi, walifukuzwa kazi baada ya kugundulika wanajihusisha na vitendo vya ujambazi kwa kushirikiana na majambazi.

“Kwa ujumla, watuhumiwa hao pamoja na kujihusisha na uhalifu, pia wanajihusisha na biashara ya dawa za kulevya, ikiwamo bangi bangi, cocaine na mirungi,” alisema Kamanda Mutafungwa.

Aliwataja watuhumiwa waliokuwa askari kuwa ni Elihuruma Mringi na Jakson Nzenzule, ambaye inasemekana anatuhumiwa kumuua mwendesha bodaboda aliyefahamika kwa jina la Nkassi Massawe, mkazi wa Rombo, mkoani hapa.

Watuhumiwa wengine ni Maris Masamu (38), Saidan Massawe (39), Godwin Mahenge (32), Baraka Kimario (23) na Lightness Wilfred (29) ambao wanatuhumiwa kwa makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha, kusuka mipango ya uhalifu  pamoja na mauaji.

Wengine ni Hilda Kihiyo (21), Elisayuni  Eskael (28), Rahel John (38), Sabina Rubei (30), Elizabeth Mtui (33) na Zacharia Mlaki (22) wanaotuhumiwa kuuza bangi na dawa nyingine za kulevya.

Katika hatua nyingine, Kamanda Mutafungwa alisema wamefanikiwa kuwakamata watu wawili raia wa Kenya kwa tuhuma za utapeli walioufanya katika Benki ya CRDB, Tawi la Moshi mjini.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Edward Kimata (53) na Chrispin Kanyuela (36), wakazi wa Nairobi nchini Kenya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles