32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Kivuli cha Lowassa chamtesa Kikwete

kikwete

Na Bakari Kimwanga, Dodoma

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete, amekumbuka matukio yaliyotokea wakati wa mchakato wa ndani wa kumpata mgombea urais wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

Kutokana na hali hiyo, alisema mchakato huo ni wa kihistoria kwake na ulikifanya chama hicho kivuke salama huku akiwataka wanaokiombea kife mwaka 2020 sasa waandike wameumia.

Akizungumza mjini hapa jana wakati akifungua kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) kilichohudhuriwa na wajumbe 365 kati ya wajumbe 374, alisema kama tukio hilo liliisalimisha CCM ni wazi itazidi kuwa imara zaidi.

Licha ya Kikwete kutotaja jina kwa uwazi, lakini alikumbuka namna alivyoingia katika kikao cha NEC na kuimbiwa wimbo na wajumbe waliomtaka Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na kusema kuwa wana imani naye.

Kikwete alisema anatambua kuwa wajumbe wa NEC pamoja na majukumu mengine ndio wenye kupitisha majina ya uongozi wa juu wa chama hicho na Serikali kwa ujumla.

“Watawezaaa…..kwa kweli ni historia na raha kweli kweli maana mwaka jana tulipokutana hapa nilipoingia ukumbini wajumbe waliamua kuimba nyimbo, huku wakimtaja fulani fulani…. maadamu CCM haikuvunjika mwaka jana haivunjiki tena maana nilisimama kama mwenyekiti wa chama.

“Na pale mafisi walikaa tayari kusubiri mkono udondoke na hakuna mkono uliodondoka na CCM ilitoka salama na sasa tuko vizuri zaidi,” alisema Kikwete.

Katika kikao hicho kilichofanyika mwaka jana, wajumbe hao walisikika kwa sauti wakiimba kuwa wana imani na Lowassa kama mtu sahihi anayepaswa kuchaguliwa kugombea urais kupitia CCM katika uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana lakini jina lake lilikatwa na Kamati ya Maadili na kushindwa kufika mbele ya NEC.

Wakati wa mchakato huo, Kamati Kuu ya CCM (CC) iliwateua makada watano ambao majina yao yalifikishwa mbele ya NEC ambao ni Rais Dk. John Magufuli, aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria ambaye kwa sasa ni Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Dk. Asha-Rose Migiro, Balozi Amina Salumu Ally, January Makamba ambaye kwa sasa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.

Katika hatua nyingine, Kikwete ambaye leo anatarajiwa kukabidhi kijiti cha uenyekiti wa chama hicho kwa Magufuli, alisema kuwa alishangazwa na moja ya taarifa zilizoandikwa na gazeti moja (si MTANZANIA) ambapo mtu mmoja alinukuliwa na watu na kudai kuwa chama hicho kitakufa mwaka 2020.

“CCM haifi na haishindwi mwaka 2020 ila watashindwa wao kama walivyoshindwa mwaka jana,” alisema Kikwete.

AMFUNDA MAGUFULI

Kikwete anayeng’atuka ndani ya CCM, alitumia nafasi hiyo kumfunda mrithi wake Magufuli na kusema kwamba wajumbe wa NEC husifu mambo yanapokwenda sawa lakini huwa wakali yanapokuwa hayaendi.

Kutokana na hali hiyo, alimtaka kufanya kazi na wajumbe hao kwa kusikiliza mawazo yao kwa kuwa ndiyo chombo cha juu cha chama pale kunapokosekana kazi ya mkutano mkuu.

“Kamati Kuu husimamia shughuli za kila siku za chama na hii ni NEC, hivyo wajumbe huwa huru kutoa maoni yao hivyo wasikilize. Husifia sana mambo yanapokwenda vizuri lakini yasipoenda vizuri wanakuwa wakali.

“Ninaomba mumpe ushirikiano Magufuli ambaye muda mfupi ujao atakuwa mwenyekiti wetu, hii ni historia haijapata kutokea, mengi yalisemwa na sasa wakati umefika,” alisema Kikwete.

Pia alishangazwa na kile alichodai uwapo wa baadhi ya watu kupika uongo kuwa NEC imepanga kumpinga Magufuli asichaguliwe kuwa mwenyekiti wa chama hicho.

“Kuna watu wana viwanda vya kuzalisha uongo kila kukicha kwa lengo la kutaka kupoteza muda wa kujibu uongo wao. Na hii ya CCM kuendelea kuwa moja inawasumbua watu,” alisema.

BARAZA LA WAZEE

Kikwete alitumia nafasi hiyo kueleza mipango yake na kusema kwa sasa anajiandaa kwenda kuwa mjumbe wa Baraza la Ushauri la Wazee wa CCM linaloundwa na viongozi wastaafu.

“Hapa nitakuja kama mtanialika kwa mambo mazito kama mwaka jana, maana nakumbuka wakati ule ukiwa mwenyekiti au makamu unakuwa mjumbe wa kudumu wa CC, sasa siku moja Mzee Mkapa anakaniambia sisi tumefanya kazi kubwa inakuaje tuhudhurie vikao hadi usiku wa manane, tunahitaji kupumzika.

“Enheee baada ya hapo yalizuka maneno JK awataka wazee wastaafu ndani ya chama lakini tulifanya vile kwa maoni yao wenyewe na si vinginevyo.

“Sitakuwa nanyi tena kwenye vikao vya NEC, hiki ndicho kikao changu cha mwisho. Mtakuwa na mwenyekiti wetu Rais Magufuli na nitakuja pale tu nitakapoalikwa na NEC,” alisema Kikwete kabla ya kikao hicho cha NEC kupitisha jina la Magufuli kuwania uenyekiti na leo ataomba kura mbele ya Mkutano Mkuu wa CCM.

VIPEPERUSHI KILA KONA

Katika hatua nyingine, jana katika mji wa Dodoma vilikuwa vinasambazwa vipeperushi mbalimbali vikiwataja wabaya wa Magufuli waliokuwa katika mkakati wa kumkwamisha asiwe mwenyekiti wa CCM.

Vipeperushi hivyo vilikuwa vikitawanywa na vijana ambao hawakuwa tayari kutaja majina yao, walikuwa wakivisambaza huku majina ya Membe, mfanyabiashara Saidi Lugumi pamoja na mwenzake, Gharib Said, wakitajwa kuwa katika mikakati ya kushawishi wajumbe wa mkutano mkuu kumpinga Magufuli kuwania uenyekiti.

Mbali na majina hayo, pia wametajwa vigogo kadhaa wa CCM wakiwamo wa CC ya sasa inayomaliza muda wake pamoja na wale wa mkutano mkuu.

MSINDAI KUREJEA CCM

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Mgana Msindai pamoja na wenzake kadhaa leo wanatarajiwa kurejea ndani ya chama hicho.

Kutokana na taarifa hiyo gazeti hili lilizungumza na Msemaji wa CCM, Christopher ole Sendeka na alithibitisha kina Msindai kurejea.

“Si Msindai tu wapo wengi mtawaona wakirejea CCM wameandika barua za maombi, tumezitafakari wapo waliokubaliwa na wengine bado wanaendelea kuchujwa na mtawaona aidha kwenye mkutano wa kesho (leo) au baada ya hapo kwa utaratibu ambao tutakuwa tumeupanga,” alisema Sendeka.

Msindai alijiengua CCM yeye pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja, ambao wote kwa pamoja walijiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwenda kumfuata Lowassa aliyeteuliwa na chama hicho kugombea urais.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles