KAMPUNI ya simu ya Zantel kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), wamezindua upya huduma ya kununua umeme kwa kutumia huduma ya Ezypesa visiwani Zanzibar.
Huduma hiyo inayojulikana kama ‘Tukuza’, ilisitishwa miezi michache iliyopita kutokana na hitilafu za kiufundi lakini sasa imeboreshwa zaidi kuweza kuhudumia wateja wengi zaidi na kwa ufanisi mkubwa.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Zantel, Benoit Janin, alisema jana kuwa Zantel itaendelea kuwa mstari wa mbele kutoa huduma zitakazorahisisha maisha ya wateja wake.
‘Tangu Kampuni ya Millicom ilipoingia, tuliahidi kuboresha huduma zetu, lakini pia kuhakikisha huduma hii ya ‘Tukuza’, inaanza kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa na leo tuna furaha kuizindua huduma hii tena, kwa uwekezaji tulioufanya tunaamini hakutakuwepo na hitilafu tena’, alisema Janin.
Mkurugenzi Mtendaji wa ZECO, Hassan Ali Mbarouk, alisema kuboreshwa kwa huduma hiyo ni hatua muhimu ya kuwawezesha wateja wa visiwa hivyo kupata huduma bora na pia kuongeza kipato kwa mawakala wa Ezypesa.
“Kupitia simu zao za mikononi, wateja wetu wataweza kutumia huduma ya Ezypesa kununua umeme na kulipia bili zao, mahali popote na kwa muda wowote na hivyo kupunguza gharama za kwenda kwenye vituo vya Zeco kununua umeme,” alisema Mbarouk.
Huduma ya Ezypesa pamoja na kutoa huduma ya Tukuza, pia inatoa fursa mbalimbali zikiwamo kuhamisha fedha kwenda mitandao mbalimbali pamoja na kufanya miamala kupitia Benki ya Watu wa Zanzibar, huku pia ikiwa katika mpango wa kuhalalishwa na Mufti wa Zanzibar.