31.2 C
Dar es Salaam
Sunday, December 15, 2024

Contact us: [email protected]

Bushir Rashid – Kilimo cha ufugaji samaki kimenitoa kimaisha

Akina mama wakiwa wanauza samaki waliovuliwa katika bwawa la Bushir Rashid
Akina mama wakiwa wanauza samaki waliovuliwa katika bwawa la Bushir Rashid.

Na Editha Karlo,Kagera

ULE usemi wa waswahili kuwa kwenye miti hakuna wajenzi unaonekana kwenda tofauti na wakazi wa Mkoa wa Kagera.

Mkoa wa Kagera una Ziwa Victoria, Buringo na visiwa vidogo 25 ambavyo wakazi wa Mkoa huo wamekuwa wakivitumia vyanzo hivyo kwa ufasaha kujipatia samaki kwa ajili ya kitoweo na kujipatia kipato.

Mbali ya shughuli za kilimo wakazi wengi wa Mkoa wa Kagera wanaendesha maisha yao kwa kutegemea shughuli za uvuvi ili kupata kitoweo na kujiongezea kipato.

Bushir Rashid (41), ni mkazi wa Kijiji cha Ruhanga kilichoko Wilaya ya Muleba mkoani humo, ni mvuvi wa muda mrefu ambaye sasa amejikita katika kilimo cha ufugaji wa samaki kisasa.
Mwandishi wa makala haya alifunga safari hadi Kijiji cha Ruhanga kujionea ufugaji wa samaki wa kisasa unaofanywa na mvuvi huyo.

Anasema amefanya shughuli za uvuvi ndani ya Ziwa vVictoria kwa miaka 20 huku akiwa na umri mdogo tu.

Anasema baada ya kugundua kuwa mazingira ya ziwa yameharibiwa na kusababisha samaki kupungua, aliamua kuanzisha shughuli za kilimo cha  ufugaji samaki katika mabwawa kwa kushirikiana na Julius Onesmo.

“Shughuli hii ya uvuvi niliianza nikiwa kijana mdogo, nimevua mwenyewe pia nimefanya kazi kwa watu tena uvuvi wa kawaida wa kutumia mitumbwi ya kienyeji kupiga kasia usiku kucha. Niliamua kuacha baada ya samaki kupungua.

“Tulikuwa tunaingia ziwani usiku na kushinda majini tukivua lakini tunapata samaki kidogo ndiyo maana nikaamua nianze kilimo cha ufugaji wa samaki,” anasema.

Anasema baada ya kumaliza darasa la saba katika Shule ya Msingi Ruhanga mwaka 1986, kutokana na hali ngumu ya maisha aliamua kwenda kufanya shughuli za uvuvi ambapo alitumia mitumbwi ya kasia na kulipwa kiasi kidogo na tajiri yake.

Anasema wakati akiendelea na shughuli hizo alipata fursa ya kutembelea eneo la Kajanse nchini Uganda kwa lengo la kujifunza jinsi wanavyofuga samaki kisasa na Kuhamasika.

Anasema baada ya kurudi nchini akaamua kutafuta eneo na kuanza kilimo cha ufugaji samaki kisasa.

“Mwaka 2007 mimi na mwenzangu tulipata eneo lenye ukubwa wa heka 60 huko Kimwani tukachimba mabwawa, tukaingiza maji na kupata mbegu 2,000 za samaki aina ya Sato kutoka Ziwa Victoria,” anasema Bushir.

Anasema baadae kulitokea tatizo la maji kupungua wakati wa kiangazi katika eneo hilo na mwaka 2009 waliamua kuhamishia shughuli zao katika eneo la Ruhanga lenye ukubwa wa heka 27.

Bushir anasema katika eneo la Ruhanga kwa sasa kuna samaki aina ya Sato zaidi ya 20,000 na Kambale zaidi ya 6,000 ambao ni mbegu zinazosubiri kuzalishwa.

Bushir anasema walisitisha uvuvi ziwani na kuweka mtaji wao katika ufugaji wa samaki lakini bado wakawa wanakwazwa na changamoto za gharama kubwa ya fedha za kuendesha kilimo hicho.

 

Anasema kuchimba bwawa moja la kisasa la mita 30 kwa 50 ni Sh milioni 8.5.

Anasema katika kilimo cha ufugaji wa samaki kisasa lazima uwe na uhakika wa maji, mashine za kisasa za kutengeneza chakula cha samaki, kuzalisha vifaranga, kupima uzito na urefu na vituo vya utafiti.

Anasema pia kitaalamu bwawa linatakiwa kuwa na samaki 12,000 na samaki hutumia miezi sita kukua hadi kuvunwa.

Kuhusu namna ya kuzalisha vifaranga vya samaki anasema kutotoa mayai kunachukua saa 12 na baadae mayai hayo huwekwa kwenye tanki maalum na kukaa humo kwa saa 12 pia. Baada ya kutolewa hukaa siku 15 na tayari vinakuwa vifaranga.

Bushir anasema awali alikuwa anapata ujira kati ya Sh 50,000 hadi 100,000 kwa mwezi kutokana na uvuvi wa kasia, lakini sasa anapata zaidi Sh milioni 15.5 kwa mwezi.

Anasema kuna uzalishaji wa aina nne na wote una faida; “Kuna kuuza vifaranga na kila kifaranga kimoja cha samaki aina ya sato kinauzwa kwa Sh 300 wakati sato wakubwa kilo moja huuzwa kati ya Sh 3,000 hadi 4,000.

Anasema vifaranga vya samaki aina ya kambale kimoja kinauzwa kati ya Sh 80 hadi 120 ambapo kambale mkubwa huuzwa kwa Sh 5,000 hadi 10,000 kutegemea ukubwa wa samaki.

Anasema vifaranga vya kambale pia vinatumika kama chambo cha kunasia samaki katika ziwa ambapo kambale wanane wanaweza kuzalisha vifaranga 500,000 hadi milioni moja kwa mwezi.

Bushir na mwenzake chini ya kampuni yao ya J&B Fish Culture Co Ltd, anasema samaki wanaovuliwa katika mabwawa yake wananunuliwa hasa na wafanyabiashara kutoka mikoa ya Arusha na Dar es salaam.

“Nina malengo ya kununua magari ya kusambaza samaki sehemu mbalimbali pia majokofu makubwa ya kisasa ya kuhifadhia samaki,” anasema.

Hata hivyo pamoja na mafanikio waliyonayo wana malengo ya kufikisha mabwawa 50 ambapo sasa yapo 36 na kuvuna samaki aina ya sato zaidi ya 1,700 kwa siku.

 

Anasema kuwa pia mabwawa yake yamekuwa yakitumika kama chuo cha watu kujifunza ufugaji wa samaki katika mabwawa na wengine kwenda kutalii.

“Hata sasa hivi wapo wanafunzi wametoka Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA), wamekuja kufanya utafiti hapa,” anasema.

Ofisa Uvuvi wa Wilaya ya Muleba, Symphori Ngaiza, anasema wapo wafugaji wa samaki 80 ambao ni binafsi na vikundi vinavyotambuliwa.

Naye Ofisa Mfawidhi Kitengo cha Ukuzaji viumbe hai majini mkoani Kagera, Erick Kiiza, anasema mkoa una mabwawa 241 ya kufugia samaki na kati ya hayo yanayomikilikiwa na serikali ni matatu na yaliyosalia ni ya watu binafsi.

Kiiza anasema wilaya inayoongoza kwa kuwa na mabwawa mengi ni Karagwe ambayo ina mabwawa 49 ikifuatiwa na Manispaa ya Bukoba 45, Bukoba vijijini 44, Muleba 41, Missenyi 28 na Ngara 25.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali mstaafu Salum Kijuu, anasema samaki wanapungua katika ziwa kutokana na kukithiri kwa vitendo vya uvuvi haramu.

Kufuatia doria zilizofanyika katika kipindi cha miaka miwili 2009/2010 na 2010/2011, wavuvi haramu 476 walikamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Pia samaki aina ya sangara wapatao kilo 23,047 na sato kilo 8,716 na zana haramu zenye thamani ya Sh bilioni 1.5 vilikamatwa na kuteketezwa kwa moto.

Zana zingine zilizokamatwa ni makokoro 503, timba 785, makila 12,965, nyavu za dagaa 293, mitumbwi ya kuvulia kokoro 495, kamba za kuvutia makokoro zenye urefu wa mita 192,274 na katuli nane.

0752202783 au email [email protected]

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles