29.1 C
Dar es Salaam
Sunday, December 15, 2024

Contact us: [email protected]

Kutoka kuuza maandazi hadi kubuni jiko la kikapu

Rehema akionyesha jiko kikapu lilivyo kwa ndani.
Rehema akionyesha jiko kikapu lilivyo kwa ndani.

Na JANETH MUSHI -MERU

“NAWASHAURI akina mama wasiopenda kujishughulisha, badala yake wanawategemea waume zao, waache tabia hiyo huu si wakati wa kubweteka na kutegemea mume, ni wakati wa kila mtu kujishughulisha ndani ya familia.”

Ndivyo anavyoanza kusema Rehema Charles (42) mjasirimali na mgunduzi wa jiko la kikapu linalopika chakula na kutumika kama chombo cha kuhifadhia ili kisipoe (Hotpot).

Rehema anayeendesha shughuli zake Mtaa wa Kwa Aloyce Maji ya Chai, Kata ya Imbaseni, Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, anasema amekuwa akijishughulisha na utengenezaji majiko yanayotumia malighafi za kuni kidogo, mabaki ya mbao, pumba za mpunga, ngano na mkaa.

Akiwa ameanzia safari ya ujasiriamali katika uuzaji wa maandazi, anasema baada ya kupata mafunzo yaliyomchukua miaka mitatu kutoka kwenye Shirika la Women Development for Science and Technology Association( WODSTA), aliamua kuchana na biashara hiyo.

Baada ya kuachana na uuzaji wa maandazi, anasema alijaribu biashara nyingine ya kutengeneza mkaa kwa kutumia karatasi, taka za miti au mbao zilizopigwa randa (maranda), pamoja na vumbi la mkaa alilomuomba jirani yake aliyekuwa anauza mkaa unaotokana na kuchoma miti.

Anasema ili kupata mkaa huo unaotokana na karatasi huwa analoweka karatasi kwenye maji kwa siku mbili na siku ya tatu huzitwanga kwenye kinu ili kuzilainisha na baada ya hapo huchanganya na vumbi la mkaa kisha kuanza kutengeneza mabonge mithiri ya maandazi na kuyaanika juani tayari kwa kutumika.

“Baada ya kufanikiwa kubuni mkaa huu, nilianza kuutumia mwenyewe ndugu na jirani waliokuwa wakija nyumbani walikuta nautumia kupikia, kidogo kidogo wakaanza kuupenda, nikajikuta naanza kuwauzia majirani zangu. Kwa hiyo soko la kwanza kabisa lilikuwa ni kwa watu wanaonizunguka.”

“Niliuza sado moja kwa Sh 700 nikafanikiwa kuuza sado tano na kuingiza Sh 3,500. Fedha hizi ndizo nilianza nazo kama mtaji wa biashara zangu, kutokana na aina ya vitu bidhaa nilizotaka kutengeneza kuhitaji mtaji,” anasema.

Rehema anaeleza kuwa baada ya kufanikiwa kukusanya mtaji huo aliamua kununua vyungu viwili, malighafi ya saruji, chokaa na mchanga zilizomuwezesha kutengeneza
majiko mawili kwa gharama ya Sh 3,500 na kuyauza kwa Sh 30,000 kwa yote mawili.

Anasema katika kuendelea na majukumu ya kutengeneza majiko hayo, alifikia uwezo wa kubuni tena aina ya jiko jingine alilolipa jina la jiko kikapu linalotumika kupikia chakula na kukihifadhi.

Rehema anasema jiko hilo amelitengeneza maalumu kwa ajili ya kupunguza gharama na kumuwezesha mtumiaji kuivisha chakula kwa gharama nafuu na kuokoa muda wa kusimamia chakula chake.

Akielezea namna linavyotengenezwa na kuivisha chakula, anasema kwanza hutengeneza kikapu kisha huingiza mfuko wa plastiki ndani yake na kujaza taka za mbao, baada ya hapo huzungushia kitambaa cheusi kwa lengo la kuhifadhi joto.

JIKO KIKAPU 5 MKAA

“Hili jiko unaweza kupika chakula cha aina yoyote isipokuwa kusonga ugali. Unaweza kupika maharagwe, makande au wali, jambo muhimu ni kuzingatia ukubwa wa sufuria yenye mfuniko ambao hautatoa mvuke nje, kwa sababu jiko hili linapika kutokana na kutengeneza joto.

“Unapotaka kupika makande au kuchemsha maharagwe kwa kutumia jiko hili, ni vyema kwanza angalau kwa nusu saa, kisha yabandike kwenye jiko jingine la mkaa, gesi au umeme ili yaanze kuchemka na kupata joto baada ya hapo ondoa na dumbukiza kwenye jiko kapu kisha funika, yataendelea kuiva yenyewe taratibu,” anasema Rehema.

Anasema mbali na jiko kapu kutumika kwa ajili ya kupikia, pia linaweza kutumika kama hotpot kwa kuhifadhia chakula kilichopikwa na kukifanya kiendelee kuwa na joto kwa muda wa saa nane bila kupoa.

“Jiko kapu lina uwezo wa kutumika kwa miaka mitano bila kuharibika wala kubadilishwa kitu chochote. Na bei yake kwa hapa nayauza kuanzia Sh 18,000 mpaka Sh  20,000. Mpaka sasa nimefanikiwa kuuza majiko 20 na wateja wangu ni watu wa kawaida kabisa,” anasema Rehema.
Anasema pamoja na kuonekana kuwavutia watu wengi, lakini bado kasi ya ununuwaji imekuwa ndogo kutokana na watu wengi kutamani kwanza kuona jiko hilo linawezaje kuivisha chakula.

Anasema kutpoka mtaji wa Sh 3,500 sasa hivi umekua na kufikia zaidi ya Sh 500,000 huku akiwa amejiunga katika vikundi vya kuweka na kukopa ambapo faida kiasi anayopa baada ya kuuza majiko huipeleka kwenye kikundi kwa ajili ya kuwekeza fedha zake.
Rehema anasema ujasiriamali huo wa kutengeneza majiko kwa sasa umemuwezesha kuondokana na utegemezi.

Kuhusu changamoto anazokabiliana nazo katika biashara hiyo, anasema kwanza ni ukosefu wa masoko ya uhakika ya kuuzia bidhaa anazotengeneza na jinsi ya kujitangaza ili watu waweze kumfahamu.

“Nakabiliwa na changamoto ya masoko, jinsi ya kufikisha bidhaa sokoni, kwani nimekuwa nikitamani kupeleka mikoani lakini inakuwa ngumu kutokana na gharama kuwa kubwa hasa ya usafirishaji.

“Watu wanaharibu sana mazingira ikiwamo kukata miti kwa ajili ya kupata kuni na mkaa. Natamani ningefika kwenye maeneo hayo ili kuwapa elimu ya kutengeneza majiko haya hatimaye kupunguza uharibifu huu,” anasema na kuongeza:

“Kwa mfano maeneo wanayolima mpunga au ngano hasa pumba za mpunga, wanaweza kuzitumia kwenye majiko haya, nimekuwa nikiishia kuangalia kwenye runinga namna pumba za mpunga zinavyochomwa moto wakati ni malighafi muhimu kwa kutunza mazingira,” anasema Rehema.
Anataja matarajio yake ya miaka mitatu ijayo kwamba ni kuwa majsiriamali mkubwa atakayefundisha vikundi mbalimbali kuhusu teknolojia hiyo inayosaidia kutunza mazingira.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles