23.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 11, 2024

Contact us: [email protected]

Mpemba – Isongole barabara inayotengewa fedha bila kujengwa

Barabara ya kutoka Mpemba wilayani Momba kwenda Isongele wilayani Ileje, ikiwa imeharibika na kusababisha wananchi kupata shida ya usafiri.
Barabara ya kutoka Mpemba wilayani Momba kwenda Isongele wilayani Ileje, ikiwa imeharibika na kusababisha wananchi kupata
shida ya usafiri.

Na Eliud Ngondo, Ileje

RAIS Dk. John Magufuli amekuwa akisisitiza juu ya nchi kuwa ya viwanda kwa kuanzia ngazi ya chini ili wakulima waweze kunufaika na shughuli zao za kilimo.

Kauli yake hiyo imekuwa mwanga kwa wananchi hususan wakulima
ambao wanaona wana nafasi kubwa ya kunufaika na kilimo tofauti na hapo awali.

Kilio kikubwa cha wananchi hao ni juu ya kupatiwa huduma ya barabara ya lami kuanzia Mpemba wilayani Momba hadi Isongole wilayani Ileje ambayo ina umbali wa kilomita 52.
MTANZANIA lilizungumza na wananchi hao ambao walieleza jinsi serikali ilivyowasahau kwa kutowasikiliza kilio chao.
Mkazi wa Ileje, Obed Kayinga, anasema:

“Kumekuwapo na ahadi za viongozi wengi wa kisiasa na wasio wa kisiasa ambao wamekuwa wakiahidi juu ya barabara kujengwa kwa kiwango cha lami lakini zimekuwa kama ni jipu.
Anasema barabara hiyo ilianza kufahamika wakati wa kipindi cha uchaguzi mkuu ambapo kila kiongozi anayeomba kura mwaka wa uchaguzi amekuwa akitoa ahadi kuwa ataijenga kwa kiwango cha lami.
Anasema wakazi wa wilaya hiyo wamekuwa wakihama kila
mwaka kutokana na shida hiyo huku kukiwa hakuna msaada wa serikali licha ya kuahidiwa kuwa itajengwa kwa kiwango cha lami.
“Mwaka 2014 Rais Magufuli alipokuwa Waziri wa Ujenzi alisema barabara itajengwa kwa kiwango cha lami kama barabara zingine lakini hadi sasa haijajengwa,” anasema.
Anaeleza mwaka jana wakati akigombea urais aliahidi kuwa barabara hiyo
itaanza mapema kujengwa kwa kiwango cha lami.
“Rais wa awamu ya tano amekuwa akisema hataki kuona ahadi zisizotekelezeka na yeye ndiye alituahidi tangu alipokuwa waziri wa ujenzi na wakati wa kuomba kura, mbona haitekelezeki,” anahoji.

Naye  Amos Mwampashi, mkazi wa Wilaya ya Ileje, anasema wilaya hiyo ni kama vile imesahaulika lakini ikifika muda wa uchaguzi inakumbukwa na viongozi wa ngazi zote hapa kuomba kupewa kura kwa madai kuwa wataijenga.

Mwampashi anasema wamekuwa wakipata shida kipindi chote kwani
muda wa masika usafiri huwa wa shida na kipindi cha kiangazi vumbi
nalo huwa ni shida.

Anaeleza kuwa wilaya hiyo imekuwa ikisahaulika sana na serikali japo kuna mpaka wa Isongole kwenda Wilaya ya Chitipa nchini Malawi lakini serikali imekuwa ikifumba macho na kuona hakuna umhimu wa kuiweka katika kiwango cha lami.

“Kuna wasomi wengi waliotoka katika wilaya hii lakini jambo la kusikitisha ni kuona wakikimbia kutokana na miundombinu ya barabara kuwa mibaya,” anasema Mwampashi.

Mwampashi anasema badala yake wamekuwa wakijenga katika maeneo mengine ambako usafiri upo.

Wengine wanakwenda mbali zaidi na kusema kuwa ziko barabara zinazojengwa kwa kiwango cha lami ambazo zina urefu mkubwa lakini yao yenye urefu wa kilomita 52 imekuwa ni wimbo usioisha.

Barabara ya Mpemba hadi Isongole haina milima itakayoigharimu serikali kwa ajili ya kupasua miamba au milima kutokana na kuwa asilimia kubwa ni tambarale.
Serikali ya Malawi kwa kutambua umuhimu wa mpaka wa Isongole wanaendelea kujenga barabara yao kwa kiwango cha lami kuja hadi mpakani mwa Isongole Tanzania.

Mkazi wa Wilaya ya Chitipa ambaye pia ni mshauri wa Rais wa Malawi, Nickson Masebo, anasema barabara ya Mpemba hadi Isongole ikijengwa kwa kiwango cha lami itafungua fursa nyingi za kiuchumi kwa wananchi wa pande zote mbili.
Anasema wao waliposikia kuwa barabara ya Mpemba hadi Isongole itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami walihamasika na kuanza kujenga ya kwao ili kuweza kukutanisha na barabara hiyo.
Anasema wananchi wanategemea kuona barabara hiyo ikijengwa kwa kiwango cha lami ili kuweza kusaidia ukuaji wa mpaka wa Isongole na kutumika kuwa njia rahisi ya kuelekea nchi za kusini mwa Afrika.

WAKUU WA WILAYA

Aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Ileje, Rosemary Senyamule, anasema mategemeo makubwa kwa wananchi wa wilaya hiyo ni kuona barabara hiyo inakuwa kwa kiwango cha Lami ili kuondokana na shida hiyo ambayo wananchi wanaipata.

Anasema barabara hiyo imekuwa na ahadi toka awamu ya nne ya uongozi wa nchi hii hadi sasa.

Anasema katika bajeti ya mwaka 2015/16 zilitengwa Sh bilioni 1.9 lakini hadi mwaka wa fedha unaisha zilikuwa hazijatolewa.

Anasema kiasi hicho cha fedha kilitengwa lengo likiwa ni kupitisha magari makubwa lakini hadi sasa wanasubiri ahadi hiyo kukamilika.

Kiongozi huyo amesema katika bajeti ya mwaka 2016/17, barabara
hiyo imetengewa Sh bilioni 16.

“Barabara hii imekuwa na ahadi nyingi sana wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 tuliahidiwa kuwa itajengwa kwa kiwango cha lami na hata Waziri Mkuu Mstafu, Mizengo Pinda wakati wa ziara yake aliahidi kuwa itajengwa,” anasema Senyamule.

Mkuu wa Wilaya ya Chitipa nchini Malawi, Grace Chirwa, anasema nchi hiyo inategemea sana Mpaka wa Isongole kwa kupitisha bidhaa mbalimbali.

Anasema jambo la ajabu ni kuona nchi ya Tanzania ambayo ilikuwa ya
kwanza kuweka matumaini ya kuwepo kwa barabara ya lami kutoka Mpemba hadi Isongole lakini bado haijaanza kuijenga.

Chirwa anaishauri serikali kutengeneza barabara hiyo kwa kiwango cha lami ili wananchi wa Malawi waweze kupitisha bidhaa zao pamoja na kurahisisha magari yatokayo nje ya nchi na kupitia Tanzania kisha kuvuka kwenda Malawi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles