33.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

Kimenuka NSSF

Crescentius Magori
Crescentius Magori

* Wakurugenzi sita, mameneja watano wasimamishwa kazi

NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

VIGOGO sita ambao ni wakurugenzi katika Shirika la Taifa la Hifadhi za Jamii (NSSF), makao makuu jijini Dar es Salaam, wakiwamo mameneja wengine watano wamesimamishwa kazi.

Wakurugenzi hao wamesimamishwa jana ili kupisha uchunguzi, baada ya Bodi ya Wadhamini ya Shirika hilo kukutana Julai 15 mwaka huu, chini ya mwenyekiti wake Profesa Samwel Wangwe.

Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na ofisi ya mkurugenzi mkuu wa shirika hilo, ilisema hatua hiyo ni utekelezaji wa taarifa za wakaguzi wa mahesabu.

“Kufuatia taarifa mbalimbali za wakaguzi wa mahesabu na shughuli za uendeshaji wa NSSF, Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii chini ya uwenyekiti  wa profesa Samwel Wangwe, katika kikao chake cha 106 kilichofanyika Julai 15, 2016, kiliagiza kusimamishwa kazi wakurugenzi sita, mameneja watano na mhandisi mmoja.

“Viongozi hao, wamesimamishwa ili kupisha uchunguzi  kubaini wahusika katika tuhuma za ubadhirifu, matumizi mabaya ya ofisi na kutofuata kanuni, sheria na taratibu katika uwekezaji, usimamizi wa miradi, manunuzi ya ardhi na ajira.

“Waliosimamishwa ni Mkurugenzi wa Mipango, Uwekezaji na Miradi, Yacoub Kidula, Mkurugenzi wa Fedha, Ludovick Mrosso, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Chiku Matessa, Mkurugenzi wa Udhibiti Hadhara na Majanga, Sadi Shemliwa, Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Mahesabu ya Ndani, Pauline Mtunda na Mkurugenzi wa Uendeshaji, Crescentius Magori.

“Mameneja waliosimamishwa ni Meneja wa Utawala, Amina Abdallah, Meneja wa Uwekezaji, Abdallah Mseli, Meneja wa Miradi, mhandisi  John Msemo, Mhasibu Mkuu, Davis Kalanje, Meneja Kiongozi, Mkoa wa Temeke, Wakili  Chedrick Komba  na Mhandisi John Ndazi ambaye ni Meneja Miradi,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Wakati hali ikiwa hivyo, mwanzoni mwa mwaka huu, Rais Dk. John Magufuli, alitengua uteuzi wa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Dk. Ramadhan Dau na kumteua kuwa balozi, ingawa hadi sasa bado hajapangiwa nchi ya kwenda kuwakilisha.

Baada ya mabadiliko hayo, mwanzoni mwa mwezi Machi mwaka huu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, alimteua Dk. Carine Wangwe kuwa Mkurugenzi mkuu mpya wa shirika hilo.

Hata hivyo, saa chache baada ya uteuzi huo, Ikulu ilitengua uteuzi huo kwa kile kilichoelezwa kuwa uteuzi wake haukufuata utaratibu.

Machi 19 mwaka huu, Rais Magufuli alimteua profesa Godius Kahyarara kuwa mkurugenzi mkuu mpya wa shirika hilo akiziba nafasi iliyoachwa wazi na Dk. Dau.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mwenyekiti wa Bodi ya NSSF, Profesa Samwel Wangwe alikiri kusimamishwa kazi kwa wakurugenzi hao.

“Wakurugenzi hawa wamesimamishwa kazi kutokana na tuhuma zinazowakabili, tumeona ni vizuri wakae pembeni wasubiri uchunguzi ukafanyike.

“ Kila mmoja wao atachunguzwa kama watabainika hawana makosa watarudi, lakini mwenye makosa sheria itafuata mkondo wake,”alisema Profesa Wangwe.

Alisema tuhuma zinazowakabili wakurugenzi hao zinatokana na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2014/2015.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles