KIGALI, RWANDA
MOROCCO imeomba kujiunga tena na Umoja wa Afrika (AU), miaka 32 baada ya kujiondoa kwenye jumuiya hiyo inayoyakutanisha mataifa ya bara hilo lenye utajiri mkubwa wa rasilimali duniani.
Ujumbe wa Mfalme Mohammed wa Sita kwenye mkutano wa kilele wa AU unaofanyika mjini hapa, unasema kuwa sasa muda umefika wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika, kuchukua nafasi yake ya kiasili kwenye familia.
Morocco ilijiondoa AU mwaka 1984, ikipinga uanachama wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Sahara Magharibi, eneo ambalo inalichukulia kuwa ni ardhi yake, na ambalo inalikalia tangu mwaka 1975.
Mara kadhaa, majeshi ya Morocco na wapiganaji wa chama cha ukombozi cha Sahrawi, Polisario Front, wamepigana kuwania udhibiti wa eneo hilo.
Mwaka 1991, Umoja wa Mataifa (UN) ulisimamia makubaliano ya kusitisha mapigano na kuahidi kuitisha kura ya maoni juu ya hatima ya Sahrawi, ingawa hadi leo haijafanyika.
Katika hotuba yake, Mfalme Mohammed ameitaka AU kufikiria upya msimamo wake kuelekea Sahrawi, akisema kwa sasa suluhisho la kisiasa linafanyiwa kazi chini ya usimamizi wa UN.