25.8 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Hatima ya Kinana mikononi mwa JPM

Rais Dk. John P. Magufuli
Rais Dk. John P. Magufuli

*CCM yakodi hoteli zote Dodoma, wajumbe 2,465 kuwasili

Na RAMADHAN HASSAN, DODOMA

HATIMA ya nani atakuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ipo mikonini mwa mwenyekiti mtarajiwa Rais Dk. John Magufuli, ambaye sasa yupo mbioni kukabidhiwa mikoba ya chama hicho.

Nafasi hiyo kwa sasa inashikiliwa na Katibu Mkuu anayemaliza muda wake, Abdulrahman Kinana, ambaye ameshika nafasi hiyo tangu Novemba, 2012.

Akizungumza na MTANZANIA jana Msemaji wa CCM, Christopher ole Sendeka, alisema hadi sasa maandalizi yanakwenda vizuri na tayari wajumbe wataanza kuwasili mjini Dodoma mapema wiki hii, kwa ajili ya Mkutano Mkuu utakaofanyika Julai 23, mwaka huu.

“Suala la nani ni Katibu Mkuu litaamuliwa na mwenyekiti mpya Dk. John Magufuli, baada ya kukabidhiwa chama na Rais mstaafu Jakaya Kikwete. Tunataraji wajumbe 2,465 watahudhuria na hata wakipungua basi ni kidogo,” alisema

Msemaji huyo wa CCM alisema kuwa baada ya Julai 23, kutakuwa na kikao cha Halmashauri Kuu ambacho ndicho kitaamua juu ya mapendekezo ya mwenyekiti mpya kama anabadili sekretarieti au laa.

“Kwa sasa Katibu Mkuu bado ni Kinana hivyo sasa hapo ndipo kuna kitandawili ambacho kitateguliwa na mwenyewe Rais Magufuli kama ataendelea na aliyepo sasa au atakuja na mtu mwingine,” alisema Sendeka.

Alipoulizwa kuhusu kuibuka kwa kundi la watu wanaompinga Rais Magufuli, asipigiwe kura kwa ajili ya kukabidhiwa chama, alisema hakuna kitu kama hicho zaidi ya taarifa hizo kuenezwa kwenye mitandao ya kijamii.

“Suala la kuwepo kwa watu kumpinga Rais Magufuli asikabidhiwe chama si geni, ingawa hadi sasa hatujaweza kumfahamu mwanachama yeote anayeendesha mpango huu.

“Mambo haya nahisi kuna kikundi cha watu kinajifurahisha katika mitandao ya kijamii hivi inawezakana vipi wajumbe walewale waliomchagua Magufuli awe mgombea wa CCM eti leo hii wageuke na kumpinga?

“… hili si kweli na si geni kama unakumbuka hata mwaka 2002 wakati mzee Benjamin Mkapa anawania uenyekiti kwa mara ya pili mambo kama haya yalijitokeza na wale waliokuwa wanatajwa walikanusha na haohao ndiyo wakawa mstari wa mbele kuhakikisha wanatafuta kura za kutosha,” alisema Sendeka.

Hata hivyo hadi sasa bado Kinana amekuwa akipewa nafasi ya kuendelea kuwa katibu mkuu ingawa mwenyewe amekuwa akitajwa na watu wake karibu kuwa anahitaji kupumzika.

Hoteli zafurika

Jana gazeti hili lilizunguka katika hoteli na nyumba mbalimbali za kulala wageni mjini hapa na kushuhudia baadhi ya matangazo yakieleza waliopanga kutakiwa kuhama ifikapo Julai 22, mwaka huu.

“Karibu mji mzima wa Dodoma hoteli zimejaa na kikubwa hapa kuna mkutano wa CCM ambapo jana wamekuja kulipia karibu zote. Hivyo kama unahitaji chumba hapa ukae lakini ikifika tarehe 22, inabidi upishe wenyewe watakuwa wamefika,” alisema mmoja wa wahuduma wa hoteli moja mjini hapa.

Naye Mashaka Kijoti, ambaye ni mmiliki wa Hoteli ya G7 iliyopo Makole alisema wageni wanaokuja mkoani hapa wanatakiwa kujipanga kwani vyumba vyote vimechukuliwa.

Wenye nyumba wapangisha

Kutokana na nyumba za wageni kujaa wageni wamiliki wa nyumba za kawaida katika eneo la Nkuhungu wamepanga kuhama katika nyumba zao ili kuwaachia wageni hao.

Juma Matola,  alisema anachoangalia kwa sasa ni fedha, hivyo yupo tayari kupanga nyumba yake kwa ajili ya wageni watakao kuja.

“Mjini nimetumwa fedha nitapangisha nyumba yangu hata kama nitalala nje ni kwa siku kadhaa tu si vibaya,’’ alisema

Polisi wachimba mkwara

Akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa, Mrakibu Mwandamizi wa jeshi hilo mkoani hapa Mayala Towo,  alisema polisi wamejipanga kuufanya Mkoa wa Dodoma kuwa kisima cha amani wakati wote na baada ya Mkutano Mkuu wa CCM.

“Amani itakuwepo wana Dodoma na Watanzania wasiwe na wasiwasi ukija na nia mbaya tutakachokufanya utawasimulia wenzako kwani kwetu amani ni wajibu wetu,” alisema Mayala.

Alitoa angalizo kwa wale watakaopokea na kuwaweka wageni katika nyumba zao ambao lengo lao ni kufanya  fujo kuwa jeshi hilo litawachukulia hatua kali za kisheria.

“Usiwe sehemu ya tatizo, kama unampokea mtu na kumweka kwako ili aje afanye vurugu wa kwanza kuchukuliwa  hatua utakuwa wewe mwenye nyumba,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles