Patricia Kimelemeta, Dar es Salaam
WATU 10 wakiwamo raia wawili wa Guinea wamepandishwa kizimbani kwa mashtaka matatu ya uhujumi uchumi baada ya kukutwa na vipande 660 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh bilioni 4.5.
Wakili wa Serikali, Paul Kadushi, alisoma hati ya mashtaka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi, Dk Yohana Yongolo.
Aliwataja watuhumiwa kuwa ni Ally Shariff na Fatoumata Saumaolo raia wa Guinea,Victor Mawalla, Calist Mawalla, Solomoni Kuhembe, Haruna Abdallah’ Kasa’, Abas Hassan ‘Jabu’,Ismail Kasa, Khalfan Kahengela na Musa Ligagabile.
Alidai   washtakiwa hao kwa pamoja,   Aprili 6, 2016 hadi 23 Juni, 2016  Dar es Salaam, waliratibu na kusafirisha vipande 660 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh bilioni 4.5 mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinyume na sheria ya wanyama pori.
Alidai   shtaka la pili linalowakabili washtakiwa hao ni   kujihusisha na nyara za Serikali kinyume na sheria ya wanyamapori ambako Juni 23 mwaka huu  Dar es Salaam walisafirisha vipande hivyo.
Katika shtaka la tatu,   washtakiwa watano kati ya hao walidaiwa walikutwa na vipande vya meno ya tembo kinyume na sheria za wanyamapori.
Kadushi alidai   upelelezi wa shauri hilo bado unaendelea na kuiomba mahakama hiyo kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kutaja.
Washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu lolote kwa madai kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza shauri hilo.
Hakimu Yongolo aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 28 mwaka huu itakapotajwa tena na washtakiwa walirudishwa rumande.