WAZAZI ni watu muhimu mno katika ujenzi wa tabia za watoto wao. Kama ambavyo mbegu za uzazi ndizo huungana kutengeneza kijusi ambacho huja kuwa mtoto, ndivyo ambavyo malezi na mwenendo mzima wa maisha katika nyumba yao hutengeneza tabia za aina yoyote kwa watoto wao.
Ukiondoa tofauti ndogo ndogo, watoto wote wangeweza kuwa na tabia moja iwapo wangekuzwa katika mazingira yanayofanana. Tofauti ya tabia tunazoziona leo, zinatokana na tofauti ya malezi/mazingira baina yetu.
Kuna wazazi, hasa wanaume, ambao hujiona kuwa na mamlaka yasiyo na mipaka kiasi kwamba wanayo hiari ya kuamua chochote nyumbani pasipokusikiliza wengine. Ni madikteta wanaoweza kuwakunjia ndita wake zao mbele ya watoto wao. Na ikibidi kwa kufoka foka kwa sababu wanayo orodha ndefu ya madai kwa watu wengine kuliko wanavyotoa wao. Mara nyingine, hata katika mambo yanayomhusu mtoto mwenyewe moja kwa moja, bado wanaendesha udikteta kwa amri zisizohojiwa.
Wapo wazazi ambao ni wagumu katika kuwasifu watoto wao pale wanapofanya jambo fulani kama ilivyotakiwa. Kwao, mtoto hata siku moja hawezi kufanya kitu sahihi na kwamba hastahili pongezi kwa chochote. Na hata anapofanya vyema, huo ni wajibu usiostahili pongezi. Kwa lugha nyepesi wanamchukulia kama kifaranga fulani hivi.
Wazazi wengine ni wanasheria-ngumu, kila kitu sheria, kuvaa sheria, kulala sheria, kula sheria, kuoga sheria. Sheria sheria sheria. Na sheria zenyewe zimeundwa pasipo kumshirikisha huyo anayetungiwa hizo sheria. Kinachohitajika ni utekelezaji basi! Pengine ulikulia katika malezi ya namna hii ama na wewe ni mzazi wa sampuli hii.
Tabia za watoto, zinatupa habari za udhaifu ama ubora wa malezi ya wazazi husika. Kwa maana rahisi kila mtoto anatengenezewa tabia na wazazi/mzazi wake. Mkandarasi wa tabia zangu kwa kiasi kikubwa ni mzazi wangu. Injinia wa sehemu kubwa ya tabia yako ni mzazi wako. Na tuangalie kwa kifupi.
Ikiwa wazazi walikuwa na aina ya malezi ya sheria ngumu ngumu, wakikushurutisha kufanya mambo bila hiari yako, ni wazi kuwa ufahamu wako utajenga dhana ya kutokujiamini kwa maana ya kwamba eti wewe si aina ya mtu awezaye kufanya kitu na watu wakakikubali. Matokeo yake unakuwa mtu anayejishuku kwa kila unalolifanya ukijiuliza uliza jinsi watu wanavyokuchukulia. Ndio maana ukisimama mbele za watu unashindwa kujiamini kwa sababu ya kufikiri zaidi hadhira hiyo inakuonaje. Ninazungumzia aibu.
Itaendelea wiki ijayo….