25.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 9, 2024

Contact us: [email protected]

Kubakwa, kulawitiwa kwa watoto kumefikia hali mbaya

Rape

Na Veronica Romwald, Dar es Salaam

KADRI miaka inavyozidi kwenda mbele, hali ya ulinzi na usalama wa mtoto Tanzania inazidi kuwa mbaya, jambo ambalo linadhihirisha kuwa zinahitajika juhudi nyingi zaidi kumlinda.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anadhihirisha hilo kwa kusema matukio ya ubakaji watoto yameongezeka kwa kiasi kikubwa.

Anasema mwaka 2015 matukio hayo yalifikia 2358 wakati mwaka 2014 yalikuwa 422. Hali hiyo ilifanya vitendo hivyo kuwa tishio kwa watoto nchini.

Anasema asilimia 49 ya unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya watoto hufanyika majumbani, wakati asilimia 23 hufanyika njiani wakati wa kwenda au kutoka shule na asilimia 15 hufanyika shuleni.

“Hali inatisha na kukera, kwani ndani ya miezi mitatu mwaka huu yaani Januari hadi Machi, matukio 1765 yameripotiwa katika vituo mbalimbali vya polisi,” anasema Ummy.

Anasema serikali kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Masuala ya Watoto (UNICEF), ilifanya utafiti kuangalia hali halisi ya ukatili dhidi ya watoto na kubaini kuwa wasichana watatu kati ya 10 na mvulana mmoja kati ya saba, wamefanyiwa ukatili wa kingono kabla ya kutimiza miaka 18.

Utafiti huo pia umeonyesha  kuwa wasichana wanne kati ya 10 na wavulana watatu kati ya 10 wamefanyiwa ukatili zaidi ya mara tatu kabla ya kufikisha miaka 18, na wasichana sita kati ya 10 wamefanyiwa ukatili ndani ya familia zao. Wakati msichana mmoja hadi wawili wamefanyiwa na walimu wao.

“Msikubali kuwalaza chumba kimoja watoto wa kike na ndugu wa kiume, kwani tabia hizo chafu zimekuwa zikifanywa na watu wa familia. Vitendo vya ubakaji na  ulawiti kwa watoto vina athari kubwa katika ustawi wa watoto,” anashauri.

Anasema serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri ya kisera na kisheria katika kusimamia utekelezaji wa haki ya mtoto kuishi, kulindwa na kuendelezwa. Pia kufanya mabadiliko ya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 inayohalalisha mtoto wa miaka 15 kuolewa kwa ridhaa ya wazazi na wa miaka 14 kwa kibali cha mahakama,” anasema Ummy.

Ni kwa msingi huo, MTANZANIA limewatafuta Chama cha Uzazi na Malezi (Umati) na kuzungumza nao ili kupata maoni yao juu ya sababu zilizochangia kuongezeka kwa vitendo hivyo nchini.

Ofisa Uhusiano wa Umati, Josephine Mugishangwe, anasema hali hiyo inachangiwa zaidi na kitendo cha wazazi kuyapa ‘mgongo’ masuala la malezi ya watoto.

“Kitendo cha wazazi kuwaachia dada wa kazi majukumu ya kulea watoto wao kinachangia mno kuongezeka kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia na kingono nchini,” anasema.

Ofisa Uhusiano wa Umati, Josephine Mugishangwe
Ofisa Uhusiano wa Umati, Josephine Mugishangwe

Mugishangwe anasema inasikitisha kuona kwamba wazazi wengi wameacha jukumu la malezi kwa dada wa kazi kwa kigezo cha kutafuta maisha, jambo ambalo si sahihi.

“Wazazi siku hizi hawajishughulishi na malezi ya watoto, jukumu lote wanawaachia dada wa kazi, wao wanaamini katika utafutaji fedha lakini haya si malezi bora kwa watoto wao.

“Ndio maana wengi hawana muda wa kukaa na watoto wao kuwaeleza kuhusu mabadiliko ya kimwili watakayokutana nayo katika ukuaji wao, hili ni somo muhimu kuwaeleza kulingana na umri wao ili waweze kujitambua na kuepuka vishawishi,” anasema.

“Umati tuna waelimishaji rika ambao huzunguka kwenye shule mbalimbali kuzungumza na watoto. Yupo mtoto mmoja wa darasa la pili aliuliza swali ambalo linastahili kuulizwa na madarasa ya juu, alihoji nini maana ya kujamiiana… tulishtuka, tukamuuliza anafahamu nini kuhusu suala hilo, akatueleza. Ilibidi tumuite mzazi wake baadae na kumueleza,” anasema.

Anasema mzazi hushauriwa kwenda na mtoto wake kwenye kitengo chao cha malezi na makuzi mara kwa mara ili waendelee kupewa ushauri zaidi.

“Tunawaita kwenye kitengo hiki wazazi ili kuwaelimisha na kufafanuliwa juu ya hatua mbalimbali za ukuaji za mtoto,” anasema.

Anasema jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba wazazi wengi wamekuwa hawazingatii kutenga muda wa kuwakagua watoto wao ili waweze kujua mapema kama wameanza kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kingono.

“Watoto wengi tunaokutana nao tumebaini kuwa wameanza kujihusisha na vitendo vya ngono huku umri wao ukiwa bado ni mdogo.

“Huwa tunalazimika kumuita mzazi wa mwanafunzi husika na kumjulisha kuhusu mtoto, huwa wanashangaa wamejulia wapi mambo hayo,” anasema na kuongeza:

“Wakati wa kumuogesha mtoto ndio mzuri kwa mzazi kuweza kumkagua kwa sababu kama anafanyiwa vibaya ni lazima atalalamika kuwa anasikia maumivu,” anasema.

Anasema wazazi pia wanapaswa kufanya uchunguzi wa kutosha kabla ya kuafiki kumpeleka mtoto wake kwenye shule ya kulala, kujua historia yake kabla ya kumpeleka mtoto.

“Wanapokwenda kuwatembelea pia wasiishie tu kuzungumza nao, ni vyema wawakague kwenye miili yao,” anasema.

Anasema Umati imekuwa ikikutana na kamati za kulea watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu, kuwapa elimu ya namna ya kuwafikia na kuwaelimisha vijana.

“Siku hizi kuna ongezeko la wasichana kujifungua wakiwa na umri mdogo, tuna programu ya kukutana nao na kuwaelimisha kuhusu uwajibikaji wa mzazi kwa mtoto wake,” anasema.

Mugishangwe anasema elimu ya mahusiano na mawasiliano hasa katika kipindi hiki cha utawandawazi inahitajika kupelekwa shuleni.

“Elimu hii siku hizi imefinywa, watoto hawajui hatua za kujitambua, mambo mengi wanajifunza huko kwenye mitandao ya kijamii.

“Wanapata wapenzi kwenye mitandao, wanawasiliana na wanakwenda kushiriki ngono ndio maana hata idadi ya walio na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi inaongezeka,” anasema.

Anasema ni lazima watoto waelezwe wazi ili waweze kubainisha uhusiano mwema ni upi na mbaya ni upi.

“Wakati umefika pia kwa serikali kuruhusu wasichana wenye umri wa miaka 25 nao wapimwe saratani ya shingo ya kizazi, kisheria ni kuanzia miaka 30 lakini wapo ambao waliliridhia kupimwa na kukutwa wamepata saratani hii.

Naye Muelimishaji Rika wa Umati, kituo cha Temeke, Kassim Abdalah, anasema ni vema wazazi wakajenga utamaduni wa kuwa karibu na watoto wao kama marafiki.

“Hii itasaidia wao kuwa wa wazi na kuwaeleza kila kitu wanachokutana nacho huko wanakopita, si kuwaachia jukumu hili wadada kwa sababu maisha ya sasa ni tofauti na zamani,” anasema.

Anasema watoto ni rahisi kujifunza vitu vingi hata visivyokuwa na faida kwao kupitia mitandao ya kijamii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles