ISTANBUL, SYRIA
WAZIRI Mkuu wa Uturuki, Binali Yildirim amesema nchi yake ina nia ya kujenga na kuimarisha uhusiano wake wa kidiplomasia na nchi jirani ya Syria.
Katika kauli ya kushangaza, alisema Uturuki nia hasa ni kujaribu kuboresha uhusiano bora na majirani zake wote.
Hii inazua picha tofauti kwani Uturuki imekuwa ikiwa miongoni mwa mataifa yaliyo mstali wa mbele kusaidia waasi na kushinikiza kung’olewa madarakani kwa utawala wa Rais wa Syria Bashar al-Assad.
Vyombo vya habari vinasema kuwa wanadiplomasia wa Uturuki na Syria wamefanya mazungumzo kadhaa katika siku za hivi karibuni.
Katika wiki za karibuni, Uturuki imemaliza uhasama na Israel pamoja na Urusi na kujenga upya uhusiano wao.
Uturuki ilikuwa imeingia katika mzozo wa kidiplomasia na Urusi ilipoangusha moja ya ndege zake za kivita iliyokuwa ikifanya doria katika mpaka wake na nchi hiyo.
Kitendo hicho mbali ya kuikasirisha Urusi, kiliifanya ilipe kisasa kwa kuzuia raia wake kuzuru Uturuki na kuiwekea vikwazo vingi vya kiuchumi.
Sekta ya Utalii nchini Uturuki ikaporomoka kwa vile inategemea zaidi watalii kutoka Urusi.
Hata hivyo, hivi karibuni Uturuki aliomba radhi hadharani kwa tukio hilo lililosababisha kifo cha rubani mmoja.