Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
KAMPUNI ya TBL Group imeahidi kuendelea kuwaunga mkono vijana wa Tanzania kwa kuwawezesha kupata elimu ya ufundi stadi katika vyuo vya Veta kupitia mpango maalumu wa kupata elimu zaidi ya vitendo kuliko nadharia unaojulikana kitaalamu kama ‘Dual Apprenticeship programme’.
Mpango huo unaoendeshwa na Serikali kupitia taasisi zake za mafunzo ya ufundi kwa kushirikiana na Chama cha Wenye Ujuzi cha Hamburg, Ujerumani.
Mpango huo umelenga kuwapatia vijana elimu na mafunzo kwa vitendo ambapo watasoma huku wakiwa wanapatiwa mafunzo ya vitendo kwenye viwanda na taasisi mbalimbali.
Akizungumzia mpango huo ulioanzishwa miaka mitatu iliyopita, Meneja wa Mafunzo wa TBL Group, Gasper Tesha, alisema umeonyesha maendeleo mazuri na makubwa ikiwa ni pamoja na kuwanufaisha vijana hao katika utendaji kazi sehemu mbalimbali kutokana na ujuzi waliopatiwa.
Tesha alisema vijana wanne waliofadhiliwa na kampuni hiyo na kupatiwa mafunzo katika fani ya umeme wa viwandani, wameweza kupata maarifa makubwa ya kazi kwa vitendo kwenye kiwanda cha TBL cha Ilala na baada ya kuhitimu masomo wameajiriwa.
“Hivi sasa kumekuwepo dhana ya waajiri wengi kuangalia vyeti badala ya ujuzi, hali ambayo kwa fani ya ufundi kunahitajika mafunzo ya vitendo kwa kiasi kikubwa ili wahitimu wa mafunzo hayo waweze kukubalika kwenye soko la ajira. Changamoto hii ni kubwa hapa nchini kwa kuwa wahitimu wengi wa fani za ufundi wanakuwa na mafunzo ya nadharia tu na wanapopata ajira wanashindwa kumudu kazi walizosomea na kukidhi matakwa ya waajiri wao,” alisema Tesha.